Habari Mseto

Wakenya wanne wajinyakulia tuzo muhimu ya kimataifa

August 16th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

[email protected]

VIJANA wanne Wakenya wameibuka washindi katika shindano la Future Leaders Connect linaloandaliwa na shirika la Uingereza kuhusu mahusiano ya kiutamaduni na nafasi za elimu ambapo watapata nafasi ya kuzuru Bunge la Uingereza mnamo Oktoba kwa mafunzo ya juu kuhusu uongozi.

Bi Sharon Adhiambo, Bw Alphaxrd Gitau Ndung’u, Bi Faith Nafula Wafula na Dkt Phyllis Maina walitangazwa washindi miongoni mwa wawaniaji wanane kutoka Kenya baada ya kuridhisha jopo la majaji kwa muda wa dakika sita kuhusu jinsi mawazo yao ya uundaji sera yangefanya taifa lao na ulimwengu kwa jumla kuwa mahali pema zaidi.

Bw Alphaxrd Gitau Ndung’u ambaye aliibuka mshindi katika shindano la Future Leaders Connect lililoandaliwa na Baraza la Uingereza. Picha/ Mary Wangari

Wanne hao walitangazwa washindi katika awamu ya tatu ya shindano la Future Leaders Connect kupitia sera zao kuhusu Huduma ya Kimsingi ya Afya, Mimba za Vijana Chipukizi, Dhuluma za Ngono na Jinsia katika Shule pamoja na Kuimarisha Makundi ya Wakulima mtawalia katika hafla iliyoandaliwa Chuo Kikuu cha Nairobi, mnamo Alhamisi, Agosti 8.

“Mtazamo wa kimataifa ni muhimu kwa viongozi wote wa siku za usoni katika mataifa yote ili kuwawezesha kuelewa na kushinda changamoto zinazoletwa na mabadiliko yanayotokea katika ulimwengu wetu. Future Leaders Connect husaidia kizazi kijacho cha viongozi kubuni ujuzi wa kisera na kufahamu watu wengine katika nyanja za kimataifa ili kuwawezesha kufanya mabadiliko chanya kote duniani. Tayari tumewaona washiriki wa awali wakichangia pakubwa katika kuwapa motisha vijana walio shuleni na kuwasaidia kujiandaa kwa changamoto za maisha baada ya elimu yao na sina shaka kwamba kundi la mwaka  huu litajitolea vivyo hivyo kukabiliana na changamoto zinazokanbili ulimwengu wetu leo. Ninatazamia kuwapokea washindi wa Kenya London mnamo Oktoba,” alisema Sir Ciarán Devane, Mkurugenzi wa Baraza la Uingereza.

Kupokea mafunzo

Kufuatia ushindi huo, Wakenya hao sasa watajiunga na kundi la washindi 50 waliochaguliwa miongoni mwa wawaniaji 15,000 kote ulimwenguni ambapo watapata fursa ya kuzuru Uingereza mnamo Oktoba 2019 kupokea mafunzo ya kiwango cha juu kuhusu uongozi katika Taasisi ya Møller, Chuo Kikuu cha Cambridge.

Aidha, watapata nafasi ya kukutana na wabunge katika Bunge la Uingereza na viongozi wengine wa kimataifa kujadili sera zao.

Future Leaders Connect ni mtandao wa viongozi waundaji sera chipukizi uliobuniwa 1934 na unaofadhiliwa na Uingereza.

Mpango huu unaojumuisha watu wenye ujuzi maalum wenye umri kati ya miaka 18-35 kote ulimwenguni ambapo wanachama wake hupatiwa nafasi ya kubuni ujuzi wao wa uundaji sera, kutangamana na watu muhimu na kupata ujuzi wa kufanya mabadiliko halisi.