Habari Mseto

Wakenya wanunua kwa wingi tiketi za VVIP kukaa pamoja na TD Jakes

September 5th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

ITAKUGHARIMU Sh 75,000 kupata nafasi ya kuketi kwenye chumba kimoja na Askofu wa kutoka Amerika Thomas Dexter Jakes Sr, anayejulikana kama TD Jakes.

Licha ya baadhi ya Wakenya kulalamika kuwa kiwango hicho cha pesa ni ghali mno, tiketi za watu mashuhuri zaidi (VVIP) tayari zimeuzwa zote.

Kulingana na waandalizi wa hafla hiyo, tiketi zilizokuwa zimesalia kufikia siku ya Jumatano ni zile za VIP.

Baadhi ya watu mashuhuri wanaotarajiwa kufanikisha hafla hiyo ni pamoja na TD Jakes, Strive Masiyiwa, na Nunu Ntshilinga.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hafla hiyo ya SOAR Africa katika mkahawa wa Villa Rosa Kempinski, TD Jakes amesema kuwa hafla hiyo ndio ya kwanza kufanyika nchini na inatarajiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya biashara.

Afisa Mkuu wa Masuala ya Wateja katika Kampuni ya Safaricom Bi Sylvia Mulinge (kushoto), Askofu wa kutoka Amerika TD Jakes (kati) pamoja na Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya KCB, Joshua Oigara. Picha/ Magdalene Wanja

“Kama mkurugenzi mkuu wa kampuni ya TD Jakes, ninaelewa hatua na mikondo mbalimbali ambayo biashara huchukua na jinsi inavyoweza kubadilisha maisha,” akasema TD Jakes.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya KCB, Joshua Oigara alisema kuwa hafla hiyo ni mwanzo wa mazungumzo na midahalo ambayo italeta mabadiliko katika uongozi.

“Naamini kwamba baadhi ya suluhu za matatizo barani Afrika zitaletwa na vijana ambao wanaweza kuwa wabunifu wakipewa nafasi,” alisema Bw Oigara.

Tiketi za kawaida zinauzwa Sh25,000 huku zile za VIP zikiuzwa Sh50,000 kila moja.

Hafla hiyo inafanyika Septemba 5, ambapo wafanyabiashara wataungana na TD Jakes kwa chajio na Ijumaa, Septemba 6 kutakuwa na hafla ya siku nzima katika ukumbi wa Kasarani.