Wakenya waona giza dhidi ya Indonesia tenisi ya Davis Cup ikianza

Wakenya waona giza dhidi ya Indonesia tenisi ya Davis Cup ikianza

Na GEOFFREY ANENE

WANATENISI wa Kenya wameanza vibaya mashindano ya Davis Cup ya dunia ya Kundi II dhidi ya Indonesia baada ya Sheil Kotecha na Ismael Changawa kubwagwa katika mchezaji ya mmoja kwa mmoja mjini Jakarta, Ijumaa.

Mchezaji anayeorodheshwa nambari moja katika tenisi nchini Kenya Sheil alikuwa wa kwanza kuingia uwanjani dhidi ya Christopher ‘Christo’ Rungkat.

Uzoefu wa miaka 10 wa Rungkat katika mashindano haya ulishuhudia akinyamazisha Sheil kwa seti 2-0 za 6-1, 6-2 akitumia saa moja na dakika tatu kupata ufanisi huo.

Changawa, ambaye alinyakua taji la mashindano ya Kenya Open mwaka 2015, 2016 na 2017, alijaribu kufufua matumaini ya Kenya bila mafanikio. Alipoteza kwa seti 2-0 za 6-2, 6-4 katika mechi iliyochukua saa moja na dakika 18.

Sheil na Changawa watapata fursa ya kunusuru kampeni ya Kenya watakapolimana na Rungkat na Christo katika mechi zingine za mchezaji mmoja kila upande hapo Jumamosi, mtawalia.

Kila timu ina wachezaji wanne. Mbali na Changawa na Sheil, Kenya pia inawakilishwa na Kevin Cheruiyot na Ibrahim Kibet Yego nayo Indonesia ina Rifqi Fitriadi na Gunawan Trismuwantara.

Indonesia inaongoza kwa mechi 2-0 baada ya siku ya kwanza. Kenya ikisawazisha kwa kushinda mechi ya mchezaji mmoja kwa mmoja mapema Jumamosi, mshindi ataamuliwa katika mechi ya wachezaji wawili kwa wawili baadaye Jumamosi.

Mshindi kati ya Kenya na Indonesia baada ya mechi hizo kuchezwa atapandishwa daraja kuingia Kundi I.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yaamuru serikali iwasilishe ripoti kuhusu virusi...

Chebukati atoa ufafanuzi kumhusu Igathe

adminleo