Habari Mseto

Wakenya wapigia simu Wabunge wakiwataka wakatae Mswada wa Fedha 2024

June 14th, 2024 1 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wameanza kampeni ya kuwashinikiza wabunge wao kukataa Mswada wa Fedha 2024 wakisema unawaumiza.

Kupitia mitandao ya kijamii, wanaharakati waliwahimiza Wakenya kuwapigia simu wabunge wao kuwataka wasipitishe mswada huo kuwa sheria.

Mwanablogu Amerix alianza kwa kuandika katika X akiwataka Wakenya kuelewa kuwa, asilimia 60 ya mapato yao ni makato ya ushuru.

“Asilimia 60 ya mapato yako huwa ni ushuru. Ni nani unafanyia kazi. Unafanyia kazi serikali. Wewe ni mtumwa. Kataa kuwa mtumwa. Chukua simu yako sasa na upigie mbunge wako. Mwambie akatae Mswada wa Fedha,” aliandika na kutoa orodha ya nambari za simu za wabunge kadhaa.

Wito wake huo ulichangamkiwa na Wakenya ambao walitoa nambari zaidi za wabunge.

“Mpigie Bw Ndindi Nyoro, Mbunge wa Kiharu. Mtumieni jumbe na kumpigia simu akatae Mswada wa Fedha. Mkumbusheni kwamba, alichaguliwa kuwakilisha na kuwa sauti ya watu wa Kiharu. Kiharu ina haki ya kumpigia simu mbunge wao,” aliandika katika X.

Baadhi ya Wabunge ambao nambari za simu zilichapishwa ni za wabunge Silvanus Osoro, Gideon Kimaiyo, Mohammed Tubi, Peter Salaysa, Patrick Simiyu, Dan Wanyama, Reuben Kiborek, John Paul Mwirigi, Kimani Ichungwa, Jessica Mbalu, Wambugu Maina. Orodha hiyo iliendelea kuwa ndefu huku nambari za simu za mamia ya wabunge zikitolewa hadharani.

Katika X, mwanablogu mmoja alichapisha zaidi ya nambari 30 za simu.

“Wasumbueni kwa simu, msikubali wabunge wenu wapate usingizi. Jazeni simu zao na jumbe. Ni lazima watekeleze majukumu waliyochaguliwa kutekeleza ambayo ni kutuwakilisha,” Karen Ngari alihimiza katika X.

Akionekana kukubaliana na Wakenya, Seneta wa Narok aliandika katika X. “ huu ndio wakati.”