Habari Mseto

Wakenya wasafiri mashambani licha ya onyo la serikali

December 22nd, 2020 1 min read

Titus Ominde na Benson Matheka

VITUO vingi vya mabasi mijini vilishuhudia ongezeko la abiria wanaosafiri maeneo ya mashambani kwa sherehe za Krismasi.

Miongoni mwa wanaosafiri ni ni wanafunzi ambao wameanza kufunga shule baada ya muhula wa pili kukamilika.

Vituo vya magari katika miji ya Nairobi, Mombasa, Nakuru, Eldoret na Kisumu vilikuwa vimefaa watu wakielekea maeneo mbali mbali ya nchi kwa sherehe za krisimasi.Hii ni licha ya serikali kuwahimiza watu wanaoishi mijini kutosafiri mashambani kuzuia maambukizi ya corona.

Katika jiji la Nairobi nauli ya kuelekea maeneo tofauti imeanza kupanda.Uchunguzi wa Taifa umebaini kuwa baadhi ya magari mengi ya uchukuzi wa umma yameweka hatua kali za kuzuia kuenea kwa janga la Covid-19.

‘ Tunahakikisha kuwa abiria wetu wanaosha mikono kabla ya kupanda na kudumisha umbali unaohitajika katika magari yetu, ”akasema Bw Jackson Mathai mhudumu wa basi mjini Eldoret.

Bi Alice Namikoye ambaye alikuwa akisafiri kutoka Eldoret kwenda Chwele katika Kaunti ya Bungoma alisema kwamba alifika katika kituo cha kuabiri magari asubuhi lakini hakuwa amepata matatu kwa sababu ya foleni ndefu.