Michezo

Wakenya washinda Istanbul Marathon

November 10th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAKENYA Bernard Cheruiyot na Diana Chemtai walitawazwa mabingwa wa Istanbul Marathon nchini Uturuki mnamo Novemba 9, 2020.

Cheruiyot alisajili muda bora wa binafsi baada ya kukata utepe kwa saa 2:11:49 kwa upande wa wanaume. Alifuatwa na Mkenya Felix Kimutai (2:12:00) ambaye alimpiku Zewudu Hailu Bekele wa Ethiopia aliyeridhika na nafasi ya tatu baada ya saa 2:12:23.

Chemtai alitamalaki mbio za upande wa wanawake kwa kusajili muda wa saa 2:22:06 mbele ya Waethiopia Hiwot Gebrekidan (2:24:30) na Tigist Memuye (2:37:52) waliokamata nafasi za pili na tatu mtawalia.

Katika mbio tofauti zilizojumuisha wanariadha wazawa wa Uturuki pekee, Yavuz Agrali alitawala kitengo cha wanaume na kuibuka mshindi wa Turkish Marathon baada ya saa 2:19:23. Tubay Erdal aliyeambulia nafasi ya sita katika mbio za jumla awali, aliibuka mshindi wa mbio za Turkish Marathon kwa upande wa wanawake baada ya saa 2:41:11.