Habari Mseto

Wakenya wasifu hatua ya korti kuzima amri ya NHIF

March 10th, 2019 2 min read

Na ANITA CHEPKOECH

WAKENYA wamefurahia hatua ya Mahakama Kuu kutupilia mbali amri ya hazina ya bima ya kitaifa ya afya (NHIF) kwamba wanandoa waliotoa hati kiapo iliyoidhinishwa na mahakimu pekee, na sio mawakili, kuthibitisha ndoa yao ndio watasajiliwa.

Mnamo Februari mwaka jana NHIF ilisema kuwa haitatambua vyeti vya ndoa vilivyoidhinishwa na mawakili.

Ilisema kuwa kanuni hiyo mpya inalenga kuzuia visa ambapo watu fulani wamekuwa waliwasajili vimada, wapenzi na watu wengine wasiostahiki kufaidi kutokana na huduma zinazotolewa na bima hiyo. NHIF ilisema kuwa pesa za umma zimekuwa zikipotea kupitia ulaghai kama huo.

Hata hivyo, Jaji John Mativo mnamo Jumanne alifutilia mbali kanuni hiyo na kuamuru kuwa vyeti vilivyoidhinishwa na mawakili vile vile vikubaliwe na NHIF kama idhibati ya uhusiano wa kindoa.

Akitoa uamuzi huo jijini Nairobi, Jaji Mativo alisema kuwa NHIF haina mamlaka ya kuamuru hati ambayo inapasa kukubalika.

“Mawakili ni maafisa wa mahakama na Katiba imewapa mamlaka ya kupeana na kusimamia viapo,” Jaji Mativo akasema.

“Washtakiwa hawana mamlaka ya kisheria kuamua stakabadhi zipi wakili aliyetawazwa anapaswa kuidhinisha au kutoidhinisha. Uamuzi uliotolewa na mshtakiwa haujahimiliwa katika sheria,” akaeleza.

Uamuzi huo umesifiwa na wananchi, wakiwemo Bi Margaret Shawitsa na Mabw Godfrey Sang na Nicholas Mburu, ambao walihisi kuwa hatua hiyo ya NHIF iliwazuia watu wengi kupata huduma za afya na kuwasumbua Wakenya wanaosaka hati za ndoa.

Akiongea na Taifa Leo, Bw Sang alisema kulingana na Sheria ya Ndoa, cheti sio ithibati ya kipekee ya kuonyesha watu wameoana na kwamba watu wawili ambao wameishi kwa zaidi ya mwaka mmoja wanaweza kuchukuliwa kuwa wameoana ikiwa hilo litathibitishwa na wasimamizi wa kiapo, wakiwemo mawakili.

“Madai ya NHIF yanachukulia kuwa mawakili hawaaminiki na wataweza kuidhinisha watu wawili kuwa wameoana kutokana na hamu ya fedha, bila kufahamu kuwa madai yao ni ya uwongo. Hatua ya kuwazuia mawakili kama hawa kuidhinisha mahusiano ya ndoa itawazuia Wakenya wengi kupata huduma za afya,” akasema Bw Sang.