Wakenya ‘wasukuma’ juu bei ya mafuta TZ

Wakenya ‘wasukuma’ juu bei ya mafuta TZ

Na IAN BYRON

MADEREVA kutoka Kenya ambao wamekuwa wakikimbia nchini Tanzania kununua mafuta, walishtuka baada ya vituo vya kuuza petroli katika nchi hiyo kuongeza bei kutokana na kuongezeka kwa mahitaji.

Vituo vya kuuza petroli mjini Sirare vimeongeza bei hadi Sh137.15 kutoka Sh98.30 baada ya madereva kutoka Kenya kufurika huko kununua mafuta kwa bei nafuu.

Mnamo Septemba 15, serikali ya Kenya, kupitia Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (Epra), iliongeza bei za mafuta kwa Sh7.58 hadi Sh136.30 kwa lita, jambo lililofanya baadhi ya madereva nchini kuandamana.

Madereva kutoka kaunti za Kisii, Homa Bay na Migori wamekuwa wakivuka mpaka hadi Tanzania kununua mafuta kabla ya wauzaji katika nchi hiyo jirani kuongeza bei.

Awali, bei ya petroli aina ya Supa ilikuwa kati ya Sh95 na Sh97, dizeli iliuzwa kwa Sh91.15 na bei ya mafuta taa ilikuwa Sh88.35 mjini Sirare kabla ya wamiliki wa vituo hivyo kuyapandisha ili kutoshana na bei ya Kenya.

Uchunguzi wa Taifa Leo Jumatatu ulifichua kwamba bei ya petroli aina ya supa iliongezeka hadi kati ya Sh137.30 na Sh138.00 katika miji ya Sirare na Tarime.

Hii imefanya madereva kutoka Kenya kutovuka mpaka kununua bidhaa hiyo.

Mwenyekiti wa chama cha wanabodaboda mjini Isebania, Bw Peter Chacha alithibitisha kwamba vituo vya kuuzia mafuta vilipandisha bei makusudi kwa sababu ya kufurika kwa Wakenya huko.

“Kuongezeka kwa madereva kutoka Kenya kumesababisha haya. Waliongeza bei ili wapate faida kubwa,” Bw Chacha alisema kwa njia ya simu.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Hofu ya ongezeko la saratani ya mapafu nchini

Kwake, fursa ya kumsalimia Mzee Jomo Kenyatta ilikuwa ni ya...