Makala

Wakenya watakuwa wakisifu na kutukana nani ili wachaguliwe 2027 Raila akienda AU?

February 26th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

IKIWA kuna kitu kimewachanganya wanasiasa wa Kenya katika harakati za Raila Odinga kuwania kiti cha mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika (AUC), ni kutoweka kwa ladha ya wasifu na matusi katika kampeni.

Iwapo Bw Odinga atatwaa wadhifa huo, itambidi akome kushiriki siasa za nchini Kenya, ikitazamiwa kwa kiwango kikuu kwamba huenda asiwanie urais 2027.

Huku walio katika ngome za Bw Odinga wakihitajika kuonekana na wafuasi wao wakimsifu na kumkinga kutokana na shutuma ili wachaguliwe, wasiompenda kinara huyo wa Azimio huhitajika kumtusi na kumdunisha.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Kanini Kega amekuwa wa kwanza kukiri kwamba ufanisi wa Bw Odinga AUC utahangaisha wanasiasa wengi.

“Mimi ninahurumia sana wanasiasa katika mirengo yote miwili. Ilichofaa kufanya ili uchaguliwe kwetu Mlima Kenya katika safari zote tano ambazo Bw Odinga amewania urais ilikuwa tu ni kumtusi na utandaze uovu wake kwa nia ya kumdunisha kwa kila kigezo. Nao wa, tuseme Nyanza, walihitajika tu kutunga nyimbo za wasifu kuhusu Bw Odinga. Akiondokea siasa za hapa kwa mujibu wa mwito wa AU, sisi tutakuwa taabani,” asema.

Bw Kega alisema kwamba “uchaguzi wa 2022 ulidhihirisha nguvu ya matusi dhidi ya Bw Odinga Mlima Kenya kwa kuwa hata mimi niliumia na nikapoteza ubunge wa Kieni kutokana na kuchagua kumsifu Odinga badala ya kumtukana”.

Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa Agikuyu Bw Wachira Kiago aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “kwa sasa itatubidi tuwe na nidhamu za kisiasa na tuzingatie masuala nyeti ya kimaendeleo kwa kuwa mbinu ya jadi ya kuchaguliwa kupitia utundu inazidi kutokomea”.

Bw Kiago alisema kwamba “sasa ni wananchi wote waungane pamoja na wazingatie masuala ya kuinua taifa hadi kwa ufanisi kwa kuwa zile siasa za ujinga na upumbavu wa kulumbana, kudunishana na kuhujumiana huku wananchi wakiwekwa kwa mirengo ya kikabila na kimaeneo zinaelekea kufika kikomo”.

Anawataka wanasiasa sasa waanze kutunga hotuba ambazo zinaongea kuhusu maendeleo, uchumi na umoja wa kitaifa.

Mbunge mwakilishi wa Kaunti ya Kirinyaga Bi Njeri Maina sasa anawaza na kuwazua itakuwaje siasa za Kenya zikipokonywa majina matamu matamu kama mganga, Baba, Jakom, Kitendawili, Mchawi, Kimundu kiguruki, Mwizi wa Sugoi, Shenzi sana, Ole Mashamba na mengineyo.

“Ni habari njema sana kwa siasa zetu kwa kuwa sasa tuna nafasi ya kuja pamoja, tuunde miungano ya kitaifa isiyo na upuzi kama wa kuchunguza kama wawaniaji wamepashwa tohara au ni wakora wa uporaji pasipo thibitisho,” akasema.

Aliyekuwa afisa wa utawala kwa muda mrefu hapa nchini Bw Joseph Kaguthi alisema kwamba “siasa zetu zinaelekea kwa mpwito ambapo ili uchaguliwe ni lazima uuze sera za maana wala sio kutandaza sarakasi”.

Alisema kwamba siasa za Kenya zinaingia katika awamu muhimu ya kizazi kipya ambacho hakielewi kuhusu historia za wakongwe wa siasa bali kinachowasumbua wapiga kura wengi wa 2027 kwa sasa kikiegemea mianya ya ufanisi.

“Ni kizazi ambacho ukikiambia Odinga ni mganga kitakuweka kwa kejeli za mitandaoni kikikuangazia kama aliyeenda kugangwa na Odinga. Ukisema mwanasiasa fulani hajapashwa tohara utajipata kwa vibonzo ukishiriki ngono naye kama ushahidi wa kule ulipata habari hizo. Waelewe mapema kwamba siasa zinaelekea kuwa na mwamko mpya,” anasema.

Aliyekuwa Gavana wa Murang’a, Bw Mwangi wa Iria alisema kwamba “kinachohitajika kwa sasa ni kuelewa mbinu za siasa zitabadilika na wanaonuia kuchaguliwa waimarishe bongo na mbinu ili kupata uwezo wa kuchaguliwa.

“Sasa hakuna wa kusifiwa na hakuna wa kutusiwa. Hekaya kwamba kulikuwa na kiapo cha jamii hii na ile zisiwahi kushirikiana kisiasa zinafika kikomo. Sasa ni kila mtu apambane na jinsi ya kuelewa masuala halisi yanayovutia wapiga kura. Kwa uhakika kuna wengi watajipapa taabani 2027 kwa kuwa siasa zinabadilika na kuwa za Kisayansi,” akasema.

 

[email protected]