Michezo

Wakenya watawala Mexico City Marathon

August 25th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Duncan Maiyo na Vivian Kiplagat wamefagia mataji ya makala ya 37 ya mbio zakilomita 42 za Mexico City nchini Mexico, Jumapili.

Katika mbio hizi zilizovutia wakimbiaji 25, 000, Maiyo alikuwa nyuma ya Mkenya mwenzake Mathew Kisorio aliyetawala kilomita 30 za kwanza. Maiyo alimpita Kisorio kama umeme baada ya kilomita ya 40 na kukata utepe kwa saa 2:12:52.

Kisorio, ambaye alikuwa amepigiwa upatu kutwaa taji kwa sababu ya muda wake bora katika marathon (saa 2:04:53), alivunjika moyo kupitwa baada ya kuongoza kwa muda mrefu pamoja na kufungua karibu mwanya wa sekunde 43 wakipita kilomita 30 na kufifia kabisa.

Kisorio alisahau kuwa jiji hilo liko mita 2,240 juu ya usawa wa bahari na kukimbia kwa kasi ya juu sana. Uchovu ulianza kumwingia baada ya kilomita 21 za kwanza na mambo yakamharibikia baada ya kilomita 40 ambapo alikuwa amefika akiwa karibu dakika tatu mbele ya mpinzani wake wa karibu Maiyo.

Kisorio alipitwa na kukamilisha mbio akiwa na bendeji mguuni, ripoti kutoka Mexico zikidai amepata jeraha ambalo anatumai kurejea Kenya kutibiwa.

Kiplagat, ambaye pia wachanganuzi walikuwa wamebashiri atashinda kitengo cha wanawake, alitolewa kijasho na Mkenya mwenzake Paskalia Kipkoech. Walikuwa bega kwa bega kwa muda mrefu kabla ya Kiplagat kufungua mwanya mdogo katika kilomita za mwisho na kumuacha kabisa na kunyakua taji kwa saa 2:33:28.

Muda wa Kiplagat ni rekopdi mpya ya Mexico City Marathon. Alifuta rekodi ya saa 2:36:12 iliyowekwa na Gladys Tejeda mwaka 2017. Kipkoech aliridhika na nafasi ya pili (2:34:09) naye Pamela Rotich akafunga tatu-bora (2:38:15). Kiplgata na Kipkoech walijitosa mbele baada ya kilomita 25 na kukimbia bega kwa bega kabla ya Kiplagat kuchukua uongozi kabisa katika kilomita ya 36.

Hii ni mara ya kwanza Kenya imeshinda mataji ya wanaume na wanawake ya Mexico City Marathon tangu Isaac Kemboi na Rose Jebet waibuke washindi mwaka 2011.

Matokeo (Agosti 25, 2019):

Wanawake

Vivian Kilpagat (Kenya) saa 2:33:28

Paskalia Kipkoech (Kenya) 2:34:09

Pamela Rotich (Kenya) 2:38:15

Zinash Debede (Ethiopia) 2:41:29

Zerfie Limeneh (Ethiopia) 2:43:27

Wanaume

Duncan Maiyo (Kenya) saa 2:12:53

Girmay Birhanu (Ethiopia) 2:16:17

Amanuel Mesel (Eritrea) 2:16:31

Yihunling Adane (Ethiopia) 2:16:43

Deribe Melka (Ethiopia) 2:21:53