Habari

Wakenya wavaa sidiria na soksi usoni wasikamatwe na polisi

April 12th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

HALI ngumu ya kiuchumi na uhaba wa maski katika maeneo kadhaa Kaunti ya Lamu, umelazimisha baadhi ya wakazi mijini na vijijini kutumia sidiria zao kujifunika midomo na pua.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulionyesha kuwa wakazi wa vijiji vya Kiongwe, Mpeketoni na baadhi ya maeneo ya Hindi wanatumia sidiria na wengine kuziba midomo na mapua yao kwa kutumia soksi na vitambaa vya kawaida, ili wajikinge kutokana na virusi vya corona.

Baadhi ya wakazi katika eneo la Kiongwe walisema hawana uwezo wa kifedha wa kununua maski.

Wafanyabiashara wanauza maski kwa kati ya Sh50 na Sh200, bei ambayo wakazi wanasema iko juu kwani biashara zao zimekwama.

Bi Diana Watuka alisema wameamua kutumia sidiria kama maski ili kuepuka kukamatwa na polisi kwa kukosa kuzivaa wakiwa hadharani.

“Maski zenyewe kwanza hazipatikani. Isitoshe, wale wachache wanaozitengeneza hapa kwetu wanatuuzia kwa bei ghali. Hali ya kiuchumi ni ngumu. Tutakimu familia zetu kwa chakula au tutanunua maski?” akauliza Bi Watuka.

Mkazi mwingine, Bi Sada Athman kutoka eneo la Hindi, alishangazwa na jinsi maski zinavyoendelea kuuzwa kwa bei ya juu licha ya serikali kutangaza awali kwamba zitakuwa zikiuzwa kwa Sh20.

Bw Johnson Mbuthia ambaye ni mkazi wa mtaa wa Bakanja, eneo la Mpeketoni, aliiomba serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuanzisha mpango wa kuwasambazia maski bila malipo wakazi ambao hawajiwezi ili kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Bw Mbuthia alishikilia kuwa maisha kwa familia nyingi za Lamu ni magumu na wakazi wamekuwa wakipata shida hata kukimu familia zao kwa chakula.

“Serikali ya kaunti na ile ya kitaifa zifikirie kuwasambazia wananchi kutoka familia zisizojiweza maski za bure la sivyo wananchi wataendelea kuvaa soksi na sidiria. Uchumi umekuwa taabu na sidhani wengi wetu tuko na uwezo wa kununua hizo maski hasa ikiwa zitaendelea kuuzwa ghali,” akasema Bw Mbuthia.

Serikali ilikuwa imesema kuwa itatoa maski kwa watu mashinani wakiwemo waendeshaji bodaboda kupitia serikali za kaunti.