Wakenya wavuma kwa wizi ng’ambo

Wakenya wavuma kwa wizi ng’ambo

NA LEONARD ONYANGO

ONGEZEKO la idadi ya Wakenya wanaohusika katika visa vya utapeli na ulaghai ng’ambo linaendelea kuharibu sifa ya Kenya kimataifa.

Hii ni baada ya Wakenya kuwa miongoni mwa washukiwa 47 waliofikishwa kortini Jumatano nchini Amerika kwa madai ya kutumia ulaghai kuiba Sh30 bilioni kutoka kwa serikali ya jimbo la Minnesota, Amerika.

Kulingana na upande wa mashtaka, Wakenya hao waliunda tovuti feki zaidi ya 300, ambazo walitumia kudai kuwa walitoa chakula cha msaada kwa watoto walioathiriwa na janga la corona kati ya 2020 na mwaka huu 2022.

Sehemu ya fedha hizo zilizoporwa nchini Amerika zilitumika kununua mali kama vile majumba, magari na vito vya thamani nchini Kenya, Uturuki na Amerika.

Wakenya hao walifikishwa kortini wiki moja tu baada ya wauguzi wawili Wakenya kushtakiwa kwa kuibia serikali ya Amerika Sh12 bilioni.

Bi Winnie Waruru, 42, ambaye amekuwa akiishi jimboni Massachusetts alikiri kuhusika na wizi huo huku mwenzake Faith Newton, 52, ambaye pia ni Mkenya, akikanusha mashtaka.

Awali Bi Kimaru na mumewe Francis Nderitu Kimaru waliibia serikali ya Amerika mabilioni ya fedha kupitia makao yao ya Compassionate Homecare.

Mnamo Juni 2022, Mamlaka ya Kutwaa Mali ya Wizi (ARA) ilinasa Sh2.3 bilioni ambazo inaaminika ziliibwa kutoka nchini Laos.

Fedha hizo zilizozuiliwa katika akaunti ya Benki ya Ecobank zinamilikiwa na raia wa Laos na Wakenya wanne.Kulingana na maafisa wa uchunguzi, Wakenya hao walishirikiana na raia huyo wa Laos kutapeli watu fedha katika nchi hiyo ya Bara Asia.

Mnamo Machi 2022, Oscar Kipikirui Ngeno, 41, alifikishwa kortini jijini New York, Amerika kwa madai ya kutapeli serikali ya Amerika Sh44.7 milioni.

Kesi hiyo ingali inaendelea jijini New York.

Agosti 2021, mhubiri Mkenya, Climate Irungu Wiseman, alikamatwa na kufikishwa kortini jijini London, Uingereza kwa madai ya kuuza dawa aliyodai ilitibu ugonjwa wa corona.

DAWA YA COVID-19

Wiseman alikuwa akiuza maji kwa Sh13,000 kwa kila chupa, akihadaa wafuasi wa kanisa lake kuwa ilikuwa dawa ya corona.

Mnamo 2019 Wakenya watatu – Robert Mutua Muli, Amil Hassan Raage na Jeffrey Sila Ndungi – walitupwa jela nchini Amerika baada kutapeli kampuni mbalimbali za nchini humo zaidi ya Sh300 milioni.

Fedha zilipotumwa walizitawanya katika akaunti mbalimbali za benki na baadaye zikatamwa Nairobi.Muli alinaswa na maafisa wa Idara ya Ujasusi ya Amerika (FBI) akiwa jijini Nairobi na akaunti yake ilipatikana na Sh212 milioni.

Mnamo Machi 25, 2021, Mkenya Florence Mwende Musau, 37, ambaye ni mkazi wa jiji la Boston, Massachusetts alikiri kushirikiana na wenzake watano kutapeli wanaume Sh400 milioni kwa kuwahadaa kupitia intaneti kuwa angeshiriki nao ngono.

Mwende alihukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani.Nchini Rwanda, Wakenya wanane walikuwa miongoni mwa watu tisa waliohukumiwa kifungo cha miaka minane gerezani mwaka 2021 kwa wizi wa Sh5.5 milioni katika Benki ya Equity nchini Rwanda.

UGAIDI

Mbali na utapeli, serikali ya Amerika inazuilia Wakenya kadhaa kuhusiana na madai ya kujihusisha na visa vya ugaidi.

Miongoni mwa wanaozuliwa ni Cholo Abdi Abdullah aliyetiwa mbaroni mnamo Disemba 2020 kwa madai ya kupanga njama ya kuteka nyara ndege ikiwa angani kwa niaba ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Ripoti iliyotolewa mwaka 2021 na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara (Unctad) inaonyesha kuwa Kenya inaongoza barani Afrika kwa kuwa kituo kikuu cha kuhalalisha pesa zinazopatikana kwa njia ya uhalifu.

Pesa hizo zinazotokana kwa utapeli, ufisadi, dawa za kulevya, ulanguzi wa fedha au binadamu hupitia Kenya kabla ya kuelekea nchi nyinginezo.

Kwa mfano, ripoti zinaonyesha kuwa fedha za kufadhili shughuli za ugaidi nchini Somalia hupitia Kenya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Unctad, Kenya iko katika nafasi ya 24 kote duniani huku Nigeria na Angola zikishikilia nafasi ya 34 na 35 mtawalia ulimwenguni.

Hali hii inafanya Kenya kumulikwa zaidi kimataifa kama kitovu cha uhalifu.

  • Tags

You can share this post!

Wakuzaji minazi nao walilia fidia

Gharama ya kustarehe yapanda – CBK

T L