Michezo

Wakenya wawili nje miaka minne kwa kutumia pufya

November 20th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KITENGO cha Maadili (AIU) katika Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), kimemwondolea marufuku Mkenya John Kibet Kendagor, ambaye alikuwa ametuhumiwa kwa kutumia dawa za kusisimua misuli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na AIU mnamo Jumatatu, Kendagor hakupatikana na hatia yoyote baada ya sampuli za damu yake kufanyiwa uchunguzi.

Mwanariadha huyo alikuwa ameshiriki mbio za marathon za Istanbul nchini Uturuki, na Seoul nchini Korea Kusini mwaka 2017, alipokezwa adhabu ya kutoshiriki mashindano yoyote yaliyofuata baada ya kukataa kutoa sampuli za damu kwa uchunguzi wa kiafya.

Afueni ya kuondolewa marafuku inamjia Kendagor siku chache baada ya Wakenya wengine Abraham Kiptum na Cyrus Rutto, kupokezwa adhabu ya kutoshiriki mbio zozote kwa miaka minne kila mmoja, kwa hatia ya kutumia pufya.

Kendagor ni bingwa wa dunia mbio za Half Marathon, naye Rutto ni bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 5,000.

Rutto na Kiptum walipigwa marufuku mnamo Aprili 4 na 26 mtawalia.

Kitum alipatikana na hatia ya kushiriki pufya mnamo Oktoba 13 mwaka jana na Aprili 26 mwaka huu. Kutokana na hilo, alivuliwa taji la kuwa mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za Half Marathon.

Aliweka rekodi hiyo katika kivumbi cha Valencia, Barcelona, katika muda wa dakika 58:18 mnamo Oktoba 28 mwaka jana.

Zaidi ya adhabu hiyo, pia amepigwa faini ya Sh5 milioni, pamoja na kwamba hatatakiwa tena kuwakilisha Kenya katika mbio zozote za kimataifa.

Wakati huo huo, Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) limewataka watimkaji kujiandaa vyema kwa kampeni mbalimbali za msimu huu wa 2019-20. Kwa mujibu wa ratiba ya AK, mapambano ya msimu huu yataanza kwa mbio za nyika zitakazoandaliwa mjini Machakos wikendi hii.

Mji wa Sotik, Kaunti ya Bomet, utakuwa mwenyeji wa makala ya pili ya mbio za nyika Desemba 14, kabla ya makala ya tatu kufanyika mjini Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua, wiki moja baadaye Desemba 21.

Makala mengine yameratibiwa kufanyika jijini Nairobi mnamo Februari 8, 2020.

Mbio hizo zitatumiwa kuteua kikosi kitakachowakilisha Kenya katika mbio za nyika za Afrika jijini Lome, Togo, mwezi Machi 3.

Mashindano ya mbio za masafa mafupi na kadri yataandaliwa na shiriko la AK mnamo Februari 22-23 mjini Eldoret, kabla ya Nairobi kuwa mwenyeji wa makala ya pili ya mbio hizo, kati ya Machi 5-6, 2020.

Uteuzi wa kikosi kitakachopeperusha bendera ya Kenya katika Riadha za Afrika jijini Algiers, Algeria, mwakani ufanyika kati ya Mei 5-8, 2020 mjini Nairobi.

Mchujo kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 ambao watanogesha Riadha za Dunia utafanyika kati ya Mei 30-31, kabla ya uteuzi wa kikosi kitakachoshiriki Olimpiki za Tokyo, Japan, kufanyika Juni 19, 2020.