Habari Mseto

Wakenya wawili watuzwa kimataifa kwa juhudi zao za kuhifadhi mazingira

August 21st, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

Wakenya wawili wametuzwa kwa juhudi zao za kuhifadhi mazingira katika Kongamano kuhusu Biashara ya Kimataifa ya Viumbehai walio Hatarini (CITES ) Geneva, Uswisi.

Wakenya hao Bw Julius Maluki Mwandai na Bw Julius Kariuki Kimani (ambaye alifariki mwaka 2018) walitambuliwa na kupewa tuzo ya hadhi ya Clark R. Bavin Wildlife Law Enforcement Award mnamo Jumanne.

Julius Maluki Mwandai ni naibu mkurugenzi mkuu wa uchunguzi katika Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS).

Kulingana na taarifa ya Taasisi ya Maslahi ya Wanyama, Bw Mwandai alipokea tuzo hiyo kwa juhudi zake za kuwashauri maelfu ya maafisa wa kitengo cha udumishaji nidhamu na utekelezaji sera katika nchi mbalimbali barani Afrika kwa miongo kadhaa.

“Juhudi zake zilichangia katika kuanzishwa kwa chuo cha KWS Paramilitary School ambacho ni chuo cha kipekee kinachotoa mafunzo ya hali ya juu na kimechangia pakubwa katika kupunguza uwindaji haramu,” ilisema taarifa hiyo.

Julius Kariuki Kimani ambaye alituzwa licha ya kwamba aliaga dunia mwezi Desemba 2018, alikumbukwa kwa juhudi zake za kuhusisha mashirika mbalimbali katika vita dhidi ya uhalifu unaowalenga wanyamapori.

“Alichangia sana katika uadilifu katika mbuga mbalimbali na utungwaji wa sheria na kanuni,” inasema taarifa hiyo.

Tangu mwaka 1997, mashirika kutoka nchi 38 yamepokea tuzo hiyo ya Clark R. Bavin Wildlife Law Enforcement Award.