Michezo

Wakenya wazidi kutesa ndondi michezo ya Afrika nchini Morocco

August 27th, 2019 1 min read

Na CHARLES ONGADI

MABONDIA wa timu ya taifa ya Kenya almaarufu ‘Hit Squad‘ waliendelea kutesa katika mashindano ya Bara Afrika (African Games) jijini Rabat nchini Morocco, Jumapili.

Watatu walitinga nusu-fainali baada ya kuandikisha ushindi mkubwa katika mapigano yao ya robo-fainali katika ukumbi wa Al Amal.

Boniface Mogunde alimkung’uta vilivyo Naftali Afonso Goma (Angola) kwa alama 5-0 katika pigano la uzani wa ‘welter’.

Mogunde sasa atazichapa na Clair Merven (Mauritius) aliyemkomoa Tswige Mmusi wa Botswana kwa alama 5-0, katika nusu-fainali.

Katika uzani wa ‘Super Heavy’, Fredrick Ramogi alitumia dakika moja pekee kumlima Firisse Mohammed (Morocco).

Ramogi anatarajiwa kupepetana na Tshikeva Kimbembi (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) katika nusu-fainali.

Kimbembi aliandikisha ushindi wa alama 5-0 dhidi ya Morais Davilson (Cape Verde).

Naye Elly Ajowi alimzaba Franklin Chukwudi Arinze (Nigeria) kwa alama 3-1 katika pigano la uzani wa ‘Heavy’.

Ajowi anayejivunia ujuzi wa miaka mingi, atapepetana na Yousef Mousa (Misri) katika hatua ya nusu-fainali.

Mambo yamwendea vibaya bondia wa kike

Hata hivyo, mambo yalimwendea mrama bondia wa kike Lorna Kusa aliyeshindwa na Shogbamu Bolante Temitope (Nigeria) kwa wingi wa alama.

Mabondia wengine wa kike wa Kenya waliojipata hoi katika mapigano yao ni nahodha Elizabeth Andiego na Everlyn Akinyi katika uzani wa kati na mwepesi mtawalia.