Habari Mseto

Wakenya wengi hawana habari wanaugua Ukimwi – Wizara ya Afya

June 6th, 2018 1 min read

Na WANDERI KAMAU

ASILIMIA 53 ya Wakenya hawafahamu kwamba wana virusi vya HIV, imesema Wizara ya Afya.

Kulingana na wizara hiyo, hili limechangiwa na wengi wao kutopimwa kwa kutofahamu umuhimu wake.

Akihutubu Jumanne kwenye uzinduzi wa mpango wa kuwahamasisha Wakenya kuhusu umuhimu wa kupimwa, Waziri wa Afya, Bi Sicily Kariuki alisema wanalenga mbinu mpya inayolenga kutoa mwelekeo mpya kuhusu vita dhidi ya ugonjwa huo.

Mpango huo unalenga kuzihoji familia 20,000 kote nchini, ambapo habari watakazotoa zitanakiliwa na kuandaa ripoti mpya kufikia mwezi Septemba.

Kufikia sasa, Wakenya 1.5 milioni wana Ukimwi, huku 1.1 milioni wakipata dawa za makali yake.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Kukabiliana na Ukimwi nchini (NASCOP) Dkt Nduku Kilonzo, kiwango hicho ni chini ya malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linaihitaji nchi husika kutoa huduma za matibabu kwa angaa asilimia 90 ya raia wake.

Kenya imeorodheshwa ya nne kote duniani kuwa miongoni mwa nchi zenye maambukizi ya juu zaidi nyuma ya Afrika Kusini, Nigeria na India.

“Tumepiga hatua kubwa, kwani kiwango cha maambukizi kimeshuka sana, sawa na idadi ya watu ambao wanaishi kwa virusi vya HIV. Hata hivyo, tunahitaji mbinu mpya kuwahamasisha watu kuhusu umuhimu wa kupimwa,” akasema Dkt Kilonzo.

Takwimu zilizotolewa pia zilionyesha kuwa eneo la Nyanza ndilo linaongoza kwa kiwango cha maambukizi, huku ukanda wa Kaskazini Mashariki ukiwa na kiwango kidogo sana cha maambukizi.