Habari Mseto

Wakfu wa Aga Khan kufaidi wakazi Kwale

May 22nd, 2019 2 min read

Na SAMUEL BAYA

WAKFU wa Aga Khan Jumatano ulisema utashirikiana na serikali ya Kaunti ya Kwale katika sekta tofauti ili kufanikisha maisha ya wakazi.

Akiongea wakati alipomtembelea Gavana wa Kaunti ya Kwale Bw Salim Mvurya afisini mwake, Afisa Mkuu Mtendaji wa wakfu huo katika eneo la Afrika Mashariki, Bw Graham Wood alisema eneo la Pwani ndilo ambalo wanalenga zaidi kutelekeza miradi yake.

Alisema kuwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Kwale ndivyo itakavyosaidia katika kuboresha maisha ya wakazi.

“Tuko na miradi mingi ambayo tunafanya katika maeneo mbalimbali nchini ila kama wakfu. Tunaangalia sana eneo la Pwani katika miradi yetu mingi ikiwemo ile ya kilimo. Kwa sasa tunalenga zaidi kuimarisha miradi hiyo katika kaunti ya Kwale,” akasema Bw Graham.

Aidha alisema kuwa wakfu huo pia utaangalia jinsi ambavyo utashirikiana na serikali ya kaunti katika miradi ambayo inalenga kuimarisha maisha ya vijana na kuwezesha akina mama katika jamii.

“Tutaangalia pia kuhusu jinsi ambavyo tunaweza kuwafundisha vijana kuhubiri amani na kuwa mfano mwema katika jamii mbali na kutayarisha mazingira bora kwa hali zao za baadaye,” akasema.

Meneja wa Wakfu huo katika eneo la Pwani Bw Atrash Ali alisema kuwa wakfu huo utalenga kuhakikisha kwamba Sh50 milioni ambazo kaunti imetenga kwa miradi ya maendeleo ya vijana zinabadilisha maisha yao.

Gavana Mvurya alifurahia ushirika huo na kutaja Wakfu wa Aga Khan kama mshirika thabiti na wa kutegemewa. Aidha alisema kuwa utawala wake umepatia kipaumbele masuala ya elimu.

“Tuko na kiasi cha Sh400 milioni ya hazina ya masomo kupitia kwa mradi wa ‘elimu ni sasa’. Katika mradi huo wanafunzi 4,300 katika shule za kitaifa na 1,800 katika vyuo vikuu wanalipiwa asimilia 100 ya karo zao na serikali ya kaunti,” akasema Bw Mvurya.

“Mbali na hilo, kila wanafunzi wa chuo cha ufundi katika kaunti hiyo hupata basari ya Sh15,000 kulipia kozi zao,” akasema Gavana Mvurya.

Aliongeza kuwa vyuo vya ufundi katika kaunti hizo vimeongezeka kutoka vyuo 11 mwaka wa 2013 had kufikia vyuo 34 kwa sasa.

“Katika upande wa afya, tumefanya maendeleo makubwa sana kwa kuboresha huduma katika hospitali ya rufaa ya Msambweni, mbali na kuboresha nyengine katika kaunti hiyo kama zile za Kinango na Samburu,” akasema Gavana Mvurya.

Gavana Mvurya aliomba Wakfu huo uendelee kuwasiaida ili kuboresha maisha ya wakazi wa kaunti hiyo.

Kaunti ya Kwale ina umaarufu kimataifa kwa vivutio vyake vingi vya utalii huku pia kukiwa na uwekezaji katika sekta za kilimo, uchimbaji madini miongoni mwa zingine.