Habari Mseto

Wakili aliyejisalimisha ICC asalia pweke Kenya ikijitenga

December 5th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

WAKILI Paul Gicheru aliyejisalimisha kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ameikosoa serikali ya Kenya kwa kukataa kumsaidia kuendeleza kesi yake.

Wiki iliyopita, serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki ilikataa wito wa ICC iliyotaka hakikisho kwamba Bw Gicheru atasaidiwa kusafiri kutoka Kenya hadi Uholanzi wakati wowote atakapohitajika mahakamani.

Bw Kariuki alikuwa amesema, Bw Gicheru hakufuata sheria kwani alihitajika kuifahamisha Mahakama Kuu humu nchini kuhusu nia yake kujisalimisha ICC na hivyo basi serikali ikiingilia itakuwa inakiuka sheria.

Msimamo huo wa serikali sasa unamweka hatarini Bw Gicheru kuendelea kukaa kizuizini The Hague, Uholanzi hadi kesi yake itakapokamilika.

Hii ni kutokana na kuwa, serikali ya Uholanzi pia haijatoa hakikisho kama itampa kibali cha kuishi katika taifa hilo kwa muda kesi ikiendelea.

Wakili wa mshtakiwa, Bw Michael Karnavas, aliambia mahakama kuwa msimamo wa serikali ya Kenya ni kinyume na matakwa ya sheria zinazosimamia ICC ikizingatiwa kuwa Kenya ni mwanachama wa mahakama hiyo.

Vile vile, alisema Uholanzi haikufuata agizo la mahakama kwani taifa hilo halikusema wazi kama litakubali Bw Gicheru aishi nchini humo wakati wa kesi yake.

“Tunaomba Jaji aagize Kenya na Uholanzi kufafanua misimamo yao kwa msingi wa sheria za ICC,” akasema Bw Karnavas.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Reine Alapini-Gansou.

Bw Gicheru anakumbwa na madai ya kushawishi mashahidi kujiondoa katika kesi iliyomwandama Naibu Rais William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Kesi ya Bw Ruto aliyekuwa ameshtakiwa pamoja na mwanahabari Joshua arap Sang ilisitishwa wakati Kiongozi wa Mashtaka, Bi Fatou Bensouda aliposema hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuiendeleza.

Bi Bensouda alilalamika kuwa, hali hiyo ilisababishwa na jinsi mashahidi aliowategemea walivyoshawishiwa kujiondoa.

Ilidaiwa mashahidi wakuu walihongwa, kupewa ahadi za ajira huku wengine wakitoweka wasijulikane waliko.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipewa uhuru wa kufufua kesi hizo baadaye endapo ushahidi mpya utapatikana.

Wakenya waliokuwa wameshtakiwa ICC kwa madai ya kuhusika kwa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, waliruhusiwa na mahakama kuja nchini wakati kesi zao zilipokuwa zikiendelea.

Wakati mwingine kesi hizo zilifanywa kwa njia ya video.

Katika kesi zinazohusu mataifa mengine, washtakiwa waliruhusiwa kuishi Uholanzi wakati kesi zao zikiendelea.

“Jaji hakuuliza Uholanzi tu kama itamsaidia Bw Gicheru kusafiri kati ya Kenya na Uholanzi, bali pia kama inaweza kumruhusu kuishi kwa muda Uholanzi wakati kesi ikiendelea,” akasema Bw Karnavas.

Hata hivyo, ICC inaweza kuomba ushirikiano wa mataifa mengine kumsitiri mshtakiwa endapo haitawezekana Kenya au Uholanzi.