Wakili ataka Jumwa amlipe Sh22.6m

Wakili ataka Jumwa amlipe Sh22.6m

Na PHILIP MUYANGA

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, anatakiwa kulipa kampuni ya mawakili Sh22.6 milioni kwa kumwakilisha katika kesi ya uchaguzi.

Kampuni ya Aoko Otieno & Associates imewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Malindi kutaka Bi Jumwa aagizwe kulipa pesa hizo.

“Pesa hizo zitaanza kuhesabiwa pamoja na ushuru kuanzia Oktoba 5, 2021,” ilani ambayo iliwasilishwa na kampuni hiyo mahakamani ilieleza.

Wakati kesi inapotamatika, wakili huandaa bili ya malipo ambayo mteja anafaa kumlipa kwa huduma zake, ikiwa mteja anaonekana mlegevu kulipia huduma hizo.

Ombi hilo huwasilishwa kwa naibu msajili wa Mahakama Kuu, ambaye hufanya tathmini ya kiwango cha pesa kilichotajwa kabla ya kutoa uamuzi kuhusu kiwango halisi ambacho wakili anastahili kulipwa.

Uamuzi unapotolewa na msajili wa mahakama, ndipo wakili ana ruhusa ya kutumia mbinu tofauti kumshurutisha mteja amlipe, kama vile kutaka mali za mteja huyo zipigwe mnada.

Mnamo Desemba 2017, Mahakama Kuu ilitupa mbali ombi la Bw Ernest Hinzano, ambaye alipinga ushindi wa Bi Jumwa kwa vile muda wa kuwasilisha ombi hilo ulipitwa na wakati.

Jaji Patrick Otieno aliamua pia kwamba, Bw Hinzano hakufuata mwelekeo unaofaa kisheria akamwagiza mlalamishi huyo kugharamia kesi kwa kumlipa Bi Jumwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) jumla ya Sh2.5 milioni.

“Kesi ninayohitajika kuamua iliwasilishwa kortini kwa njia isiyofaa na kwa hivyo haifai kwa vyovyote,” alisema Jaji Otieno, akieleza kuwa kesi hiyo haikufaa kushughulikiwa kwa vyovyote na mahakama.

Korti ilisema kesi hiyo iliwasilishwa kwa wakati ufaao lakini mshtakiwa hakuarifiwa kamwe na hivyo inaweza tu kuchukuliwa kuwa mlalamishi aliiondoa au kuisitisha hata kama haikutolewa katika faili ya korti.

Korti ilisema, badala yake, kesi iliyokabidhiwa mshtakiwa haikuwasilishwa kwa njia ifaayo kwa kukosa kulipa ada ya korti na kuiingiza katika Sajili ya Mashtaka.

You can share this post!

Umaskini wasukuma wavuvi bahari hatari

Siraj: Nitasalia Harambee Stars