Habari

Wakili augua ghafla kizimbani kabla ya kusomewa shtaka la wizi

July 31st, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI anayekabiliwa na shtaka la kuwmibia mteja wake Sh4 milioni aliugua ghafla akiwa kizimbani na kuomba kesi iahirishwe hadi Jumanne.

Bw Billy Amugune Shigoli (pichani) alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot na kuomba asisomewe shtaka kwa vile anaugua maradhi ya kisukukari na shinikizo la damu.

“Mshtakiwa huyu ambaye ni wakili anaugua maradhi ya ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu. Hatajua kile anajibu hataka akisomewa shtaka,” Bw Cheruiyiot alifahamishwa na wakili anayemtetea mshtakiwa Bw John Swaka.

Mahakama ilifahamishwa kuwa tangu mshukiwa huyo alipotiwa nguvuni hakuweza kujidunga sindano ya ugonjwa wa kisukari.

Bw Swaka alisema mshtakiwa vile vile hakuweza kutumia dawa za maradhi ya shinikizo la damu.

Aliomba mahakama iahirishe kesi hadi Jumanne kumwezesha Bw Shigoli kupata nafuu.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi hilo.

Akitoa uamuzi, Bw Cheruiyot alisema kuwa “mshtakiwa ni mgonjwa na sio utu na ni kinyume cha sheria kumsomea shtaka  kama ameeleza korti kuwa hajisikii vizuri.”

Bw Shigoli anakabiliwa na shtaka la kumwibia Bi Caroline Anne Cheledi Sh4,027,500 alizopokea kwa niaba ya mlalamishi.

Cheti cha shtaka kinasema kuwa Bw Shigoli alipokea pesa hizo kati ya Janauari 15 na Machi 7 2017 katika jengo la Embassy jijini Nairobi.

Bw Cheruiyot alimwachilia wakili huyo kwa dhamana ya Sh300,000.