Wakili kortini kwa madai ya kulaghai mayatima Sh100m

Wakili kortini kwa madai ya kulaghai mayatima Sh100m

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI alishtakiwa jana pamoja na mfanyabiashara bwanyenye kwa kuwalaghai mayatima kampuni ya wazazi wao yenye thamani ya Sh100milioni.

Wakili huyo Philemon Morara Apiemi alishtakiwa pamoja na Bw Shahdadpuri Chanshymam Choithram mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi.

Bw Choithram, hakufika kortini kama alivyoagizwa na upande wa mashtaka kwa vile anaugua ugonjwa wa Corona.

Morara alifika kortini na kukanusha mashtaka saba dhidi yake kisha akaomba aachiliwe kwa dhamana.

Wakili anayemwakilisha Bw Choithram anayeshtakiwa kuwalaghai waridhi wa mali ya marehemu Suresh Lakhian na Narian Choithram Shahdadpuri.

Morara na Choithram wanakabiliwa na mashtaka 13 ya kula njama ya kuwalaghai waridhi wa marehemu Suresh Lakhian na Narian Choithram Shahdadpuri kampuni ijulikanay- Global Apparels Kenya (EPZ) Limited-GAK (EPZ)-

“Bw Choithram hajafika kortini kwa vile ameagizwa na madaktari katika hospitali ya Aga Khan ajitenge kwa muda wa siku 14 apone ugonjwa wa Corona,”hakimu alifahamishwa na wakili wa mfanyabiashara huyo.

Mahakama iliombwa itaje kesi dhidi ya Bw Choithram katika muda wa siku 14 kumwezesha apone.

“Nitamkabidhi karani wa mahakama nakala ya ripoti hii kutoka hospitali ya Aga Khan kuhusu Bw Choithram,” Bw Andayi alielezwa.

Bw Apiemi anakabiliwa na mashhtaka saba ilhali bwanyenye huyo anakabiliwa na mashtaka 13 ya kujipatia ya kujinyakulia kampuni ya wenda zao kwa njia ya ulaghai.

Kiongozi wa mashtaka Bi Angela Fuchaka hakupinga ombi la kesi dhidi ya Bw Choithram kutengewa siku nyingine “kwa vile anaugua maradhi ya Corona.”

Wawili hao ,Choithram na Morara wanakabiliwa na shtaka la kuwafuja waridhi wa GAK (EPZ) Ltd hisa 250,000 zenye thamani ya Sh25milioni na hisa nyingine 750,000 zenye thamani ya Sh75milioni.

Shtaka lilisema Bw Choithram alijifanya kuwa Mkurugenzi wa GAK (EPZ) Ltd na Morara wakili wa kampuni hiyo ya GAK(EPZ) Ltd na kujiandikia hisa hizo zote.

Bi Fuchaka alielezea mahakama kuwa hisa hizo zilimfaidi Choithram.

Wawili hao walidaiwa walitekeleza uhalifu huo kati ya Oktoba 16 2016 na Juni 13 2018.

Morara na Choithram wanadaiwa walijiandikia cheti cha kuandikisha hisa za kampuni hiyo mnamo Juni 18 2018 wakidai hati za kubadilisha umiliki zilikuwa zimetiwa sahihi na marehemu Suresh Lakhian na Narian Choithram Shahdadpuri.

Morara alishtakiwa kuwasilisha vyeti vya kubadilisha umiliki wa kampuni hiyo katika afisi ya msajili wa makampuni afisi ya mwanasheria mkuu akidai zilikuwa halisi.

Mahakama ilimwachilia Morara kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu.

Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili ndipo Bw Choithram ashtakiwe.

You can share this post!

NASAHA: Ni muhimu kwa muumini kudumu katika kuomba msamaha

Tuungane tulinde maslahi ya Mlima Kenya – Kiunjuri