Habari

Wakili mtaalamu wa Katiba afariki ghafla

October 25th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Wataaalamu (CoE) walioandika Katiba ya sasa Wakili Philip Nzamba Kitonga amefariki baada kuugua kwa muda mfupi, familia yake imetangaza.

Kitonga, ambaye amewahi kushikilia wadhifa wa Rais wa Chama cha Mawakili Afrika Mashariki, alifariki Jumamosi, Oktoba 24, 2020, akiwa njiani akielekea Nairobi kutoka Makueni.

Alizaliwa mnamo 1956 katika Kaunti ya Kitui na amefariki akiwa na umri miaka 64.

Marehemu Kitonga pia amewahi kuhudumu katika Mahakama ya Soko la Pamoja Afrika Mashariki na Kusini (COMESA) kuhusu Haki.

Ni miongoni mwa wanasheria walioorodheshwa kuhojiwa kwa wadhifa wa Jaji Mkuu wa Kenya kuchukua nafasi ya Dkt Willy Mutunga alipostaafu mnamo 2016. Aliyefanikiwa kuteuliwa ni Jaji David Maraga ambaye pia anastaafu mapema mwaka wa 2021.

Pia amewahi kujihusisha katika siasa ambapo aliwania kiti cha Ugavana wa Kitui mnamo 2013 lakini akashindwa na Mhandisi Julius Malombe.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior ni miongoni mwa viongozi waliomwomboleza Kitonga. Kwenye ujumbe kupitia Twitter Seneta Kilonzo Junior alisema: “Nzamba ni mtu mwadilifu, mtaaalamu ambaye mchango wake katika Nyanja ya sheria nchini na barani Afrika itakoswa. Lala pema rafiki na mkubwa wangu katika taaluma ya uanasheria.”