Habari Mseto

Wakili taabani kwa kuilaghai kaunti mamilioni

May 22nd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI alishtakiwa Jumatano kwa kuilaghai Kaunti ya Nairobi zaidi ya Sh6.2 milioni.

Bi Mercy Moragwa Mogusu alikana shtaka la ulaghai mbele ya hakimu mkuu mahakama ya milimani Nairobi Bw Francis Andayi.

Mercy alidaiwa kati ya Aprili 2 2015 na Aprili 2 2018 katika afisi za kaunti ya Nairobi kwa njia ya udanganyifu alidai alipwe Sh6,234,829.65 akidai ni malipo ya kuitetea kaunti hiyo kwenye kesi kortini.

Bw Andayi alifahamishwa wakili huyo aliwasilisha maombi ya malipo akidai aliitetea kaunti katika kesi iliyoshtakiwa na kampuni ya Kiango General Supplies.

Kesi hiyo ilikuwa nambari 172/2015.

Mshtakiwa alikanusha shtaka hilo na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini mmoja wa kiasi hicho.