Michezo

Wakili wa Misri ataka Ramos atozwe fidia ya Sh120 bilioni kwa kumtendea Salah unyama

May 29th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAKILI mmoja nchini Misri sasa amewasilisha kesi kortini akitaka fidia ya Sh120 bilioni dhidi ya difenda wa Real Madrid na Uhispania Sergio Ramos kwa kumjeruhi nyota wa Misri na Liverpool Mohamed Salah kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya jijini Kiev, Ukraine.

Akitokea katika runinga moja ya Misri, Sada El Balad, wakili Bassem Wahba alitangaza kuwa amewailisha malalamishi kwa mashirika ya soka ya FIFA na UEFA akisema Ramos alimuumiza Salah kimakusudi na alimsababishia Salah ‘maumivu ya kimwili na kaiakili’ pamoja na taifa nzima la Misri.

“Ramos alimjeruhi Salah kimakusudi na anafaa kuadhibiwa kwa vitendo vyake. Nimewasilisha kesi mahakamani na malalamisi kwa FIFA.

“Ninataka fidia, ambayo huenda ikazidi Sh120 bilioni, kwa majeraha ya kimwili na kisaikolojia ambayo Ramos aliisababishia Misri na Salah,” akasema.

Hapo Jumatatu kampeni dhidi ya Ramos ilichacha mitandaoni ambapo amashabiki wanaomba FIFA na UEFA kumtia adabu Ramos. Kufikia sasa, mashabiki 300,000 wametia saini adhabu hiyo.

Ingawa Salah amesema yuko tayari kwa Kombe la Dunia, mashabiki bado wanataka kuona Ramos akikabiliwa kisheria kwa kuwa jeraha hilo lilipelekea Liverpoo kupigwa 3-1 na Real Madrid, ili kuonya wachezaji wenye tabia kama hiyo.