Habari Mseto

Wakili wa serikali ataka jopo la majaji 3 kusikiza kesi ya Mwilu

October 11th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANASHERIA wa serikali Kennedy Ogetto Jumanne aliomba kesi aliyowasilisha DCJ Philomena Mwilu ipelekwe kwa Jaji Mkuu (CJ) ateue jopo la majaji watatu kusikiza ombi la kupinga kushtakiwa kwake.

Bw Ogetto alimweleza Jaji Enock Chacha Mwita kuwa ombi la DCJ Mwilu linahoji nguvu za mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP za kuwafungulia washukiwa mashtaka.

“Kesi hii inazua masuala mazito ya kisheria kwa vile DCJ Mwilu anasema anaonewa kwa sababu ya uamuzi wa Mahakama ya Juu wa Septemba 2017 ulioharamisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017,” alidokeza Bw Ogetto.

Alisema kesi hiyo ya DCJ Mwilu inahitaji kuamuliwa na majaji watatu ndipo waweke wazi kuhusu nguvu za DPP za kuendeleza kesi.

Pia aliomba mahakama iamue iwapo kesi hiyo ya Jaji Mwilu itasikizwa na Jaji mmoja wa Mahakama kuu haki haitatendeka.

Lakini wakili Okong’o Omogeni anayemwakilisha DCJ Mwilu alisema suala linalotakiwa kuamuliwa ni “ ikiwa kukopa pesa kwa benki ni hatia ya uhalifu.”

Bw Ogetto alikuwa mmoja wa mawakili waliomtetea Rais Kenyatta katika kesi ya kupinga ushindi wake.

Aliteuliwa kuwa Wakili Mkuu wa Serikali ( SG) baada ya kutupiliwa mbali kwa kesi ya pili ya kipinga ushindi wa Bw Kenyatta baada ya uchaguzi wa pili wa urais Oktoba 2017.