Makala

WAKILISHA: Ajikakamua kufukuza ujinga barani

March 26th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

VIJANA wa Kiafrika wanaaminika kutokuwa na ari ya kusoma vitabu wakilinganishwa na wenzao kutoka sehemu zingine ulimwenguni.

Na ni dhana hii ambayo Martin Gachenge, 22, anapania kubadilisha kupitia jitihada zake za kukuza tabia ya kusoma miongoni mwa vijana.

Bw Gachenge ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo huo Kikuu cha Moi anakosomea Fasihi ya Kiingereza, anafanya hivi kupitia makujwaa mbalimbali aliyoanzisha kuwarai vijana kusoma vitabu kama mojawapo ya njia ya kuendeleza jamii.

Yeye ni mwanzilishi mshirika wa Nairobi Literary Café, mradi ambao bali na kutoa jukwaa kwa waandishi na wahariri kubadilishana mawazo, linakuza tabia ya kusoma miongoni mwa vijana.

Ikiwa ni mwaka mmoja tangu mradi huu kung’oa nanga rasmi, umesaidia waandishi kuimarisha kazi zao na kufahamu jinsi ya kutumia vipaji vyao kupitisha ujumbe thabiti wa kuleta mabadiliko katika jamii.

Ili kukuza tabia ya mazoea ya kusoma miongoni mwa vijana, wameanzisha vyama vya kusoma (book clubs) ambapo kufikia sasa wana jukwaa linalowapa wanachama fursa ya kuwasilisha maoni kuhusu masuala yanayohitaji kuimarishwa katika jamii.

Sio hayo tu, wameenda hatua zaidi na kuanzisha mpango wa kukusanya vitabu kisha kuvitoa kwa wanafunzi wanaovihitaji.

“Bado hatujakita mizizi katika sehemu zingine nchini kwani tunamakinika na Nairobi ila usimamizi wa mradi huu ungali unafanya utafiti kubaini ni wanafunzi kutoka maeneo yapi wanaohitaji msaada zaidi ambapo hivi karibuni tunatumai kuandaa shughuli ya kwanza,” aeleza Gachenge.

Hata hivyo, tayari matokeo ya jitihada zao yameanza kushuhudiwa huku maisha ya wanafunzi wengi hasa kutoka maeneo tofauti jijini Nairobi yakibadilika.

“Tumekuwa tukipata jumbe za shukrani kutoka kwa wanafunzi ambao kupitia mradi huu wamejiimarisha kimasomo, vile vile vijana ambao jukwaa hili limewasaidia kujinufaisha kitaaluma,” aeleza.

Kwa upande mwingine, yeye ni mwanzilishi mshirika wa The Discourse Journal of Literature, jarida la mtandaoni linalosambaza kazi za waandishi kuwapa mwanga.

“Kwa kawaida jukwaa hili huchapisha makala, hadithi na maoni ya waandishi na kuyasambaza,” aeleza.

Mamia wajiandikisha

Na licha ya kuwa jukwaa hili limekuwepo kwa muda mfupi tu, tayari mamia ya waandishi wamejiandikisha huku shughuli rasmi zikitarajiwa kuanza mwezi Mei.

Aidha, yeye ni mwanzilishi wa Academic club 10, chama ambacho tangu Aprili Mwaka jana kimekuwa kikisaidia wanafunzi kutambua wanachopenda kufanya, kando na masomo.

“Kwa kawaida, vikao hivi vya unasihi huandaliwa kwa siku kumi wanafunzi wakiwa likizoni,” aeleza.

Kwa sasa wanaazimia kupanua huduma za mradi huu katika maeneo mengine nchini na hasa ya mashambani na hata nchi zingine za Afrika.

“Wanafunzi wengi kutoka maeneo ya mashambani hawasomi kivyao baada ya kupata mafunzo darasani. Pia hafla nyingi za masomo hufanyika maeneo ya mijini, suala linalowatenga wanafunzi wengi wa mashambani na tulitaka kubadilisha taswira hiyo,” aeleza.

Kadhalika wanaamini kwamba kwa kusoma, raia kutoka mataifa mbalimbali barani wataweka kando tofauti zao, vile vile mipaka ya kijiografia na hivyo kushirikiana kuafikia lengo la kuendeleza bara hili.

Bw Gachenge ambaye kwa sasa anafanya majaribio ya Ualimu katika shule ya upili ya Uhuru mjini Nakuru, anasema anatumia vitabu kama chombo cha kunasua vijana kutokana na minyororo ya ujinga kama mbinu ya kukuza bara hili.