Makala

WAKILISHA: Anakuza vipaji vya uvumbuzi

March 19th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA zama hizi ambapo vijana wanahimizwa kuwa wabunifu na kujiundia nafasi za ajira, wengi wameimarisha vipaji vyao vya uvumbuzi.

Hasa wengi wamejitosa katika sekta ya uvumbuzi wa kiteknolojia na mtandao huku idadi ya apu zinazozinduliwa ikizidi kuongezeka kila uchao.

Hata hivyo, uhaba wa mbinu za kuendeleza uvumbuzi huu na hata kuwezesha bidhaa na huduma kufikia wateja wengi, ni changamoto kwa harakati hizi.

Ni hapa huduma yake Michael Karaimu, 28, inawasaidia wengi. Bw Karaimu ni mmoja wa wawakilishi wa kampuni ya FasterCapital, yenye makao yake Dubai.

Bw Michael Karaimu, 28. Picha/ Evans Habil

Kampuni hii inasaidia kutambua na kukuza vipaji hasa katika masuala ya habari na mawasiliano (IT).

Tayari Bw Karaimu amewasajili wajasiriamali kumi tangu mwanzoni mwa mwaka, licha ya kuwa alianzisha shughuli hii mwaka huu tu baada ya kuacha kazi kama mshauri wa masuala ya kifedha katika kampuni moja hapa nchini.

“Kufikia sasa tumetambua vijana wanaofanya vyema katika sekta za teknolojia katika huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia rununu, masuala ya kisheria, kifedha, kilimo na elimu miongoni mwa zingine. Pia, tunalenga wafadhili wa kibiashara, mashirika yasiyo ya kiserikali na yale ya kijamii, miongoni mwa taasisi zingine za kibiashara,” aeleza Bw Karaimu.

Ushauri

Mbali na kutambua wavumbuzi hawa, Bw Karaimu huwapa waliofuzu ushauri wa kuimarisha biashara zao kabla ya kuwasaidia kujisajili katika shirika la FasterCapital.

Na endapo bidhaa ya mvumbuzi au mfanyabiashara itakubaliwa na kumwezesha kufuzu kujiunga na kampuni hii, kazi yake itafadhiliwa, kuimarishwa na kufanyiwa matangazo.

“Katika kampuni yetu kuna wawekezaji wengi ambao wakishapata taarifa kuhusu mhusika na wafurahishwe na uvumbuzi wake, watashauriana kisha kuufadhili endapo wataridhika. Pia, hapa uvumbuzi huu utapata fursa ya kutangazwa katika wavuti wetu miongoni mwa vyombo vingine vya habari,” aeleza.

Kisha kuna wale ambao wana wazo fulani lakini bado hawajaunda bidhaa ambapo hupata usaidizi kuwawezesha kuiunda, kuifanyia majaribio mara tatu ili kuhakikisha ubora, kabla ya kuipelekwa sokoni.

“Pia hapa wahusika wanaweza kupokea huduma za kisheria, za masuala ya wafanyakazi na mauzo. Aidha, wanaochaguliwa wana fursa ya kukutanishwa na wanasihi wa hali ya juu, wamiliki wa kampuni kubwa na viongozi katika sekta mbalimbali,” aeleza.

Kwa kawaida yeye hukutana na wavumbuzi hawa kupitia mapendekezo ya wengine na warsha miongoni mwa sehemu zingine.

Kama mwakilishi wa shirika hili, kuna masuala ambayo sharti aangalie kabla ya kumsajili mvumbuzi.

“Kwa mfano lazima nijue kuhusu uvumbuzi au biashara hiyo na inaendeshwa na watu wangapi. Pia, lazima nijue mipango yako ya kibiashara ili kubaini faida zake au zinazotarajiwa kabla ya kukusajili na kukutuma kwa jopo litakalobaini iwapo umefuzu au la,” aeleza.

Anasema kwamba sio kazi rahisi na kuwa inahitaji subira, uvumilivu na maadili ya kikazi.

“Subira ni muhimu hasa ikizingatiwa kwamba hatua hizi huchukua muda kabla ya uvumbuzi kukubalika na kupata ufadhili, ndipo nami nipate ujira wangu,” aeleza.

Kwa sasa anatumai kwamba katika siku za usoni ataunda hazina ya kusimamia pesa za wawekezaji wanaofadhili biashara ndogo (venture investment fund), itakayosaidia vijana katika uwekezaji wa kiteknolojia.