Makala

WAKILISHA: Anatumia sanaa kulinda mazingira

February 26th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA ulimwengu ambapo masuala ya mazingira hayapewi kipaumbele kama yanavyostahili, amejitwika jukumu la kuhakikisha kwamba yanaangaziwa vilivyo na kufika hata maeneo ya mashinani mjini Meru.

Kinachofanya jitihada zake Bw Paul Muruingi kuwa na mashiko hata zaidi, ni mbinu anazotumia kuafikia haya.

Huku wengi wakichukulia suala la sanaa kuwa la burudani tu, Bw Muruingi ambaye pia ni mwanamuziki anayefahamika kwa jina Opus katika ulingo wa burudani, anatumia jukwaa hili kupitisha ujumbe huu wa umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Kwa takriban miaka sita sasa Bw Muruingi amekuwa akifanya hivi kupitia Music in the Park Africa (MitP Africa), tamasha ya muziki aliyoanzisha mwaka wa 2013 na ambayo imekuwa ikiandaliwa mara mbili au tatu kwa mwaka huku makala ya hivi karibuni yakitarajiwa kufanyika Mei 11.

Msanii Paul Muriungi maarufu Opus ambaye pia ni mwasisi wa Music in the Park Africa (MitP Africa). Picha/ Hisani

Kupitia mradi huu wamekuwa wakiandaa hafla za muziki ambapo wanaalika baadhi ya wanamuziki wanaosikika nchini, lakini tofauti na tamasha zingine za muziki, madhumuni makuu hapa ni kuhamasisha watu kuhusiana na umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

“Tamasha hii inatoa jukwaa kwa wanamuziki, washairi na mashabiki wao kukutana ambapo mbali na burudani, wanapata fursa ya kuangazia masuala ya kuimarisha usafi wa mazingira. Hafla hii inatoa fursa kwa mashirika na wahisani kuungana na jamii, na kuimarisha mazingira kupitia kampeni za uhamasishaji,” aeleza Opus.

Lakini hayaishii hapo tu kwani jitihada zao zinahusisha pia wao wenyewe kushirikisha jamii katika shughuli za kusafisha mazingira.

“Tamasha hii kwa kawaida huwa na awamu tatu. Asubuhi wakazi wanahusika na shughuli za kusafisha mji wa Meru, kabla ya baadaye jioni kuungana katika shoo ya muziki ambapo mashabiki wanapata fursa ya kutumbuizwa na baadhi ya wanamuziki wanaosikika nchini,” aeleza.

Mbali na hayo, pia wakati wa asubuhi kwa ushirikiano na hospitali, kampuni za bima na benki, wao huandaa hafla ambapo wakazi wanapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu bila malipo.

Umaarufu wa tamasha hii umekuwa ukidhihirika kila wakati na hata kuvutia ushiriki wa baadhi ya wanamuziki wanaotambulika sio tu mjini Meru bali pia nchini kote, kwa mfano bendi ya H_art the Band.

Na jitihada zake tayari zinazaa matunda kwani hadhira yao imeongezeka kutoka 200 walipoanza hadi 1,600 mwaka wa 2017.

“Katika makala ya mwaka 2019 yanayotarajiwa kuandaliwa mwezi Mei, tunatarajia zaidi ya watu 5,000 watahudhuria; hasa ikizingatiwa kwamba tunashirikiana na mashirika kadha,” aeleza.

Ujumbe wafika mbali

Hii, asema kwamba inamaanisha kwamba ujumbe wao kuhusiana na umuhimu wa kuhifadhi mazingira unaendelea kufikia watu zaidi.

Ni suala ambalo limewafanya kuanzisha mradi mwingine kwa jina Adopt a litter bin katika makala yajayo.

“Hapa tunaalika mashirika kutoa msaada wa mapipa ya taka ambapo sisi wenyewe tanayaweka katika sehemu mbali mbali mjini Meru katika harakati za kuzuia utupaji taka kiholela. Katika makala hayo ya mwezi Mei, tunatarajia kupata zaidi ya mapipa 4000,” aongeza.

Msukumo wa kujihusisha na masuala ya uhifadhi wa mazingira ulianza mwaka wa 2013 baada ya kukerwa na jinsi suala la utupaji taka kiholela lilikuwa kero sio tu kwa wakazi wa mji wa Meru, bali nchini kote.

“Niligundua kwamba watu wengi hawakuwa wanazingatia umuhimu wa kutupa taka mahali panapotakikana. Na kutokana na sababu kwamba mimi ni mwanamuziki, niliona sanaa hii kama jukwaa ambalo ningetumia kupitisha ujumbe huu,” aeleza huku akiongeza kwamba kwa sasa wanatumai kupanua huduma hizi katika sehemu zingine nchini.