Makala

WAKILISHA: Apanda farasi wawili kwa ustadi mkuu

July 2nd, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

LICHA ya kwamba anasomea sheria, anasisitiza kamwe hatolegeza jitihada zake za kutimiza ndoto ya kuwa mwanamuziki.

Kutana na Mildred Ouma, 21, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta na mkazi wa kitongoji duni cha Mathare number 10, ambaye anaendeleza kipaji chake kimuziki huku akisomea Uanasheria chuoni.

Ustadi wake katika muziki umemuundia jina sio tu mtaani anakoishi na kanisani, bali pia chuoni ambapo nyimbo zake zinazugusia masuala ya kawaida maishani.

“Chuoni nafahamika kwa kipaji changu cha muziki, na mtaani uimbaji wangu umenifanya kuwa maarufu na kuheshimika miongoni mwa vijana wa rika langu na hata walionishinda umri,” anasema.

Hii ni mojawapo ya sababu iliyomfanya kuwa mmojawapo wa vijana waliochaguliwa na shirika la Franky Entertainment ili kupata fursa ya kupiga msasa vipaji vyao katika usanii.

“Tulikuwa tukitafuta vipaji katika mtaa huu, na japo bado hajarejkodi muziki, nidhamu na bidii yake ilitosha kwani anaonyesha ishara za kung’aa katika siku zijazo endapo atapata usaidizi,” akasema mmojawapo wa maafisa wa mradi huu.

Mbali na muziki kuwa taaluma anayoenzi, umekuwa kimbilio lake huku ukimuepusha na maovu yanayohusishwa na vitongoji duni.

“Vitongoji duni kama Mathare huhusishwa na maovu kama vile matumizi ya mihadarati, uhalifu na ukahaba. Muziki unanifanya nitumie muda wangu kutunga nyimbo na kuzirekodi, hasa wakati ambapo siko darasani,” anaeleza.

Mildred alizaliwa mwaka wa 1998 katika kitongoji duni cha Mathare miongoni mwa watoto watano.

Alisoma na kukamilisha shule ya msingi ya Mathare Community Outreach ambapo alifanikiwa kupata alama 327 kwenye mtihani wa KCPE.

Alama hizi nzuri zilimhifadhia nafasi katika shule ya upili ya wasichana ya Nyamira Girls High School, Kaunti ya Siaya.

Alianza kuimba akiwa na miaka minane kutokana na penzi lake kwa muziki huku akishiriki katika mashindano ya muziki shuleni na kanisani. “Kuimba katika vikundi hivi kuliniepushia mengi ikiwa ni pamoja na kujihusisha na magenge mtaani,” aeleza.

Akiwa katika kidato cha pili msiba ulibisha kwao mamake ambaye alikuwa mchuuzi wa mboga alipofariki baada ya kuugua, na hivyo kumuachia babake majukumu ya malezi. Lakini hata kabla ya kupata nafuu kutokana na kifo cha mamake, babake pia alifariki.

“Pamoja na ndugu zangu, tulilazimika kujishughulikia, suala lililofanya maisha kuwa magumu zaidi. Nakumbuka ni hapa nilipozama kabisa katika muziki na kutumia uimbaji kama njia ya hifadhi hisia zangu,” anaeleza.

Bidii

Anasema kwamba nguvu alizopata kutokana na muziki zilimfanya kutia bidii kimasomo na hata kumwezesha kufanya vyema katika mtihani wa kitaifa wa KCSE mwaka wa 2015 ambapo alijizolea alama ya A- na hivyo kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Kama mwanafunzi wa sheria, anasema kwamba muziki umemuongezea ujasiri wa kusema mbele ya watu na kuonyesha hisia zake, suala ambalo linamsaidia kuwasiliana vyema.

Lakini licha ya kuzama katika muziki, hajatelekeza majukumu yake kama mwanafunzi.

“Nafahamu kwa dhati kuwa kuna wakati wa kuwa darasani na kukuza kipaji changu. Kama sasa niko katika likizo ndefu ya miezi minne na ni wakati huu ambaomimi hutumia sana kujihusisha na muziki,” anaeleza.

Anashauri vijana wenzake kutumia fursa walio nayo kutimiza ndoto zao. “Usiache umaskini ukuzuie kutimiza ndoto yako,” anaeleza.

Kwa sasa ndoto yake ni kubadilisha penzi lake kuwa taaluma.

“Napanga kupiga msasa kipaji changu kimuziki na kutumia uimbaji kama jukwaa la kunitambulisha ulimwenguni kote. Lakini pia, nafanya kila niwezavyo kuendeleza taaluma yangu ya mwanasheria,” asema.