Makala

WAKILISHA: Kipaji chao ni kwa ajili yao na jamii pia

July 23rd, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

WANAPANIA kuteka tasnia ya densi nchini Kenya; na bila Skysquad Dance Crew, wako mbioni kufikia ndoto hiyo.

Tayari kikundi hiki kinachojumuisha wanadensi wanane kati ya umri wa miaka 19 na 24 kinaonyesha ishara za kuteka tasbua hii nchini.

Wanadensi hawa ni Lucas Owuor, Daniel Muthee, Danson Mulwa, Cyrus Lochi, Antony Ewalang, Kevin Abdi, Vincent Maina na Brian Otieno ambapo wanajivunia kuafikia mengi kutokana na kipaji chao licha ya kudumu katika fani hii kwa miaka miwili pekee.

Kikundi hiki kimebobea katika kucheza aina mbalimbali za densi ikiwa ni pamoja na Dancehall, nyimbo za kisasa, densi za kitamaduni, Hip hop na Rhumba miongoni mwa zingine.

Wanachochewa na haja ya kuangazia masuala mbalimbali yanayoikumba jamii.

“Pia, nia yetu ni kuhimiza vijana hasa wale ambao hawakubahatika kufanya vyema kimasomo, kwamba huo sio mwisho wa maisha na haimaanishi kwamba hawawezi kufanikiwa maishani,” aeleza Lucas ambaye ndiye kiongozi.

Skysquad Dance Crew. Picha/ Hisani

Ustadi wao ni dhahiri huku wakiwahi kushiriki katika mashindano mengi katika sehemu mbalimbali nchini. Pia, wanajivunia kushiriki kwenye shoo kadha za haiba ya juu nchini na hata kuangaziwa na vyombo tofauti vya habari.

“Agosti 12, 2018, tulishiriki katika shindano kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana. Pia, Desemba mwaka jana tulishiriki kwenye Churchill Show,” aeleza.

Na tayari bidii yao imetambuliwa katika majukwaa tofauti kwani miezi michache baada ya kuzinduliwa, tayari walikuwa wameanza kung’aa.

“Kwa mfano, Desemba 2017 tulitambuliwa kama kikundi bora cha densi katika eneo la Bonde la Ufa kwenye shindano la densi za kitamaduni. Agosti mwaka jana, pia tulituzwa kama kikundi bora katika eneo la Laikipia,” aeleza.

Lakini mbali na tuzo, vile vile utambuzi, wanatumia densi kueleza mambo yanayohusiana na jamii kwa jumla. “Tunafunza jamii kwa kuunda densi kuhusu tatizo fulani, vile vile suluhu, ambapo tunaamini kwamba mbali na burudani, inaelimika kupitia shughuli hii,” asema.

Pia, wanasema kwamba densi imekuwa mbinu wanayotumia kujimarisha kitabia. “Kwa mfano kama mcheza densi, naweza onyesha hisia zangu, suala ambalo pia limeniwezesha kuwa na ujasiri wa kusimama na kunena mbele ya umati wa watu,” aeleza Lucas.

Kikundi hiki kilizinduliwa Mei 25, 2017 huku wanachama watatu Lucas Owuor, Daniel Muthee na Danson Mulwa wakiwa waasisi wake.

“Mimi na Daniel tulikuwa katika kikundi kimoja cha densi kilichokuwa kikijulikana kama Skillaz Dance Crew, ilhali Danson alikuwa katika kikundi cha Young Tallis,” aeleza Lucas.

Kisha Cyrus Lochi aliungana na kikundi hiki siku mbili baadaye ambapo alikuwa anajihusisha na michezo ya sarakasi na kuigiza vitabu vya riwaya.

“Miezi miwili baadaye tukiwa katika mojawapo ya ziara zetu, tulikutana na Brian Otieno ambaye alikuwa mwanachama wa kikundi cha Watrax Dance Crew,” aeleza Lucas.

Hasa ikizingatiwa kwamba walikamilisha masomo ya shule ya upili miaka michache iliyopita, bali na densi pia wajihusisha na mambo mengine.

“Baadhi yetu tunasomea kozi tofauti katika vyuo vya juu. Mimi na Brian ni wasanii ambapo tumezindua kibao Okang’ei,” aeleza Lucas.

Bado ndoto yao kuu inasalia kutambulika nchini kote kutokana na densi na kushiriki kwenye mashindano ya hadhi ya juu kama vile Sakata.

“Pia, kama Skysquad ni ndoto yetu kuwa kikundi bora zaidi duniani na tunaamini kwamba hiyo inawezekana. Pia, tunataka kukuza wanadensi wengi iwezekanavyo na kuwashirikisha kwenye kikundi chetu,” aongeza Lucas.