Habari Mseto

Wakiukaji kanuni za Covid kuosha vyoo vya umma

November 18th, 2020 2 min read

CHARLES LWANGA na MUREEN ONGALA

SERIKALI ya Kaunti ya Kilifi ikishirikiana na kamati ya usalama, imependekeza kuwa watu watakaopatikana na hatia ya kupuuza kanuni za kukabiliana na maamukizi ya corona wafanyishwe kazi ya kutoa huduma kwa jamii.

Gavana wa Kilifi Amason Kingi na Kamishna wa kaunti hiyo, Bw Kutswa Olaka, walisema wakosaji watapewa vifaa ili kusafisha mitaa, kuosha vyoo vya umma, kufyeka vichaka na aina nyingine za huduma kwa jamii.

Wakihutubia wanahabari mjini Kilifi baada ya mkutano wa kudhibiti ongezeko la Covid-19 katika kaunti hiyo, Bw Kingi alisema hatua hiyo ambayo huenda ikatekelezwa baada ya wiki mbili zijazo ni kati ya maazimio ambayo serikali kuu na kaunti zimefikiana ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

“Badala ya kujaza mahakama, vituo vya polisi na magereza, wao watapewa vifaa watoe huduma kwa jamii na kuwa funzo kwa wengine ambao wanakaidi amri za kukabiliana na mamabukizi ya corona,” alisema.

Vilevile, Bw Kingi alitangaza kuwa kamati hiyo ya kukabiliana na janga la corona imepiga marufuku uchezaji wa soka pamoja na michezo mingine ikiwemo mikutano ya kisiasa.

Ili kudhibiti maambukizi katika masoko hasa maeneo ya Malindi, Kilifi, Mariakani na Gongoni, Bw Kingi aliamuru kuwa kila soko litamteua mwakilishi wao ambaye atafanya kazi pamoja na kamati ya kusimamia masoko ili kutekeleza itifaki na kanuni za kukabiliana na maambukizi ya corona.

Kwa upande wake, Bw Olaka alisema serikali kuu inaendeleza mikutano na idara ya mahakama katika juhudi za kutatua changamoto ya msongamano katika magereza.

Alisema kuwa magereza ya Mitangani na Bofa katika kaunti hiyo yamesongamana kwa sababu ya idadi kubwa ya wafungwa kutoka kaunti za Lamu na Tana River.

Alisema tayari vilabu saba vimefungwa na kupokonywa leseni zao za kufanya kazi, watu 454 wakatiwa mbaroni kwa kutovaa barakoa na wengine 419 kukamatwa kwa kutotii masharti ya kutotoka nje baada ya saa nne usiku.

Alisihi umma kuwa katika mstari wa mbele kupigana na virusi hivi ili kupunguza maambukizi kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa na wizara ya Afya na pia kutilia maanani masharti yaliyobuniwa na serikali ya kaunti.