Habari

Wako ajitetea

November 20th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA mwanasheria mkuu nchini Amos Wako amepuuzilia mbali marufuku aliyowekewa na Amerika yanayomzuia kuzuru taifa hilo akisema hatua hiyo haitaathiri utendakazi wake kama Seneta wa Busia na majukumu yake mengine kimataifa.

Wengine waliozimwa kuingia Amerika ni mkewe Flora na mwanawe wa kiume Julius Wako kwa tuhuma za “kuhusika katika sakata kuu za ufisadi”.

Akiongea na wanahabari Jumatano katika majengo ya bunge, Nairobi Bw Wako hata hivyo ameitaka Amerika kufichua kesi za ufisadi ambazo inadai zilichangia kuwekewa marufuku hayo.

“Kuzuiwa kwangu kuingia Amerika hakuniathiri kwa njia yoyote. Hiki ni kitu kidogo sana. Maisha yangu na kazi yangu kama Seneta wa Busia, mwanachama wa Jopo la Maridhiano (BBI) na mwanachama wa Tume ya Kimataifa kuhusu Sheria hayayumbishwi na marufuku haya,” akasema Wako.

Akaongeza: “Hata hivyo ninakana madai ya Amerika nikisema kwamba sijawahi kutajwa, kushukiwa, kuchunguzwa au kushtakiwa kuhusiana na ufisadi kwa muda wa miaka 20 nilipohudumu kama Mwanasheria Mkuu nchini na baadaye nikiwa Seneta.”

Ametoa changamoto kwa Amerika kutoa habari hizo kwake na Wakenya wote “endapo inazo.”

Hata hivyo, Seneta huyo wa ODM ameungama kuwa amekuwa shahidi katika kesi mbalimbali za sakata ya Anglo Leasing iliyofichuliwa 2003.

Inakisiwa kuwa Kenya ilipoteza zaidi ya Sh43 bilioni kupitia utoaji zabuni ya vifaa vya usalama wakati wa utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki

Kulingana na Bw Wako hii sio mara ya kwanza kuzimwa kuzuru Amerika kwani taifa hilo limewahi kumzima kuingia kwa sababu ya “kushiriki ufisadi na hivyo kuhatarisha masilahi ya Amerika”.

“Kwa hivyo, nashangaa mbona nawekewa marufuku mengine ilhali sawa na niliyowekewa Novemba 4, 2009, kwa misingi ile ile miaka 10 baadaye. Nadhani njia hii ya kuniharibia jina haina manufaa yoyote katika vita dhidi ya ufisadi,” akaeleza.

Mnamo Novemba 18, 2019, Waziri wa Mashauri ya Nchini za Kigeni wa Amerika Michael Pompeo alibainisha Bw Wako amepigwa marufu kuingia Amerika kama sehemu za juhudi za kushirikiana na Kenya katika vita dhidi ya ufisadi.

“Hatua ya leo inaashiria kuwa Amerika ni mshirika mkuu wa Kenya katika vita dhidi ya ufisadi. Ustawi wa kiuchumi kwa manufaa ya Wakenya wote unaweza tu kufikiwa kwa kushinda vita dhidi ya uovu huo,” Bw Pompeo akasema kwenye taarifa iliyowekwa katika tovuti ya wizara yake.

Hata hivyo, Bw Wako amesema licha ya marufuku ya 2009 amekuwa akizuru Amerika kuhudhuria mikutano ya Tume ya Kimataifa kuhusu Sheria (ILC) ambayo ni mojawapo ya asasi za Umoja wa Mataifa (UN).

“Lakini kando na kuhudhuria mikutano ya ILC, sina shughuli zingine ambazo zinaweza kunipeleka Amerika,” akasema.

Seneta Wako pia ameishutumu Amerika kwa kujumuisha watu wa familia yake katika marufuku hiyo akisema hamna sababu yoyote ya majina yao kupakwa matope bila sababu yoyote.

“Ikiwa nilitenda uhalifu wote, madai ambayo nakana kabisa, inafaa nihukumiwe kivyangu. Mke wangu na mwanangu hawakuhusika kwa njia yoyote katika kesi zozote wakati wa hatamu yangu kama Mwanasheria Mkuu Nchini hadi nilipostaafu mnamo Agosti 2011,” akasema.