Michezo

WAKO NDANI: Arsenal kifua mbele FA

January 29th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KINGS PARK, Uingereza

KOCHA Mikel Arteta amefurahia kiwango cha makinda wake walioandikisha ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya Bournemouth, na kutinga raundi ya tano ya Kombe la FA ambapo sasa watakutana na Portsmouth.

Arsenal walijipatia mabao hayo kupitia kwa Bukayo Saka, ambaye kwa kawaida ni winga wa kushoto lakini kwa sasa anacheza kama beki wa kushoto kwa sababu ya majeraha kwa mabeki halisi.

Straika Eddie Nketiah alifunga bao la pili. Sam Surridge ambaye aliingia mahali pa Dominic Solanke aliwafungia wenyeji bao moja zikibakia dakika nane mechi hiyo kumalizika ugani Vitality Stadium.

“Nimefurahi. Ilikuwa mechi ngumu, lakini vijana walicheza kwa uelewano mkubwa na kila mtu alikuwa makini zaidi na nilifurahia sana,” alisema Arteta.

“Niliwapa nafasi kwa lengo la kuoana viwango vyao na kwa kweli nimefurahia vitu nilivyoona wakifanya uwanjani. Tulicheza vizuri zaidi hasa katika kipindi cha kwanza. Walipigana vikali, lakini tuliwalemea katika safu zote na hatimaye tukafaulu kuibuka washindi.”

Saka alifunga bao la kwanza mapema baada ya kumchanganya kipa, kabla ya Nketiah kuongeza la pili la ushindi dakika ya 26.

Arteta alitoa pongezi za binafsi kwa Nketiah mwenye umri wa miaka 20, ambaye alirejeshwa mwezi huu ugani Emirates kutoka klabu ya Leeds United alikokuwa kwa mkopo lakini haukuridhisha.

“Eddie Nketiah ni mkali. Alionekana akicheza kama winga, na sekunde chache akarejea katikati na kufunga bao. Hii imedhibitisha alivyo tayari kutufungia mabao. Mchango wake ulikuwa mkubwa uwanjani,” kocha alimsifia.

Kwa jumla, mashabiki wa Arsenala wameanza kufurahia mchezo wa kikosi chao tangu Arteta, ambaye alikuwa naibu wa Pep Guardiola pale Manchester City, atue uwanjani Emirates mwezi Desemba 2019.

Arteta alimsaidia Guardiola kuongoza City kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu (EPL), pamoja na makombe ya FA na Carabao msimu uliopita katika uga wa Etihad Stadium.

Vijana wa Arsenal wamerejelea soka yao ya nipe nikupe waliyocheza chini ya mkongwe Arsene Wenger. Kabla Saka afunge bao, mpira ulikuwa umeguzwa na wachezaji 10 wakitoa pasi zaidi ya 20.

Mchezo wa Arsenal ulikuwa umerudi chini wakati wa kocha Unai Emery aliyetimuliwa Desemba kufuatia matokeo duni.

Kocha Arteta ana makinda kadhaa ambao wameibukia kupendwa na mashabiki ikiwemo mshambuliaji Gabriel Martinelli, Saka, kiungo Willock na kiungo Matteo Guendouzi.

Katika mechi ya Jumatatu usiku, kocha Eddie Howe alilaumu wachezaji wake kwa kichapo hicho

“Tulizungmza kwa urefu wakati wa mapumziko kuhusu mchezo wetu, lakini hutukujirekebisha mapema,” akasema.

Ingawa hivyo, alisisitiza kwamba lengo lao kwa sasa litakuwa kuokoa timu hiyo ijitoe eneo hatari la kushushwa chini kutoka EPL.

Bournemouth watakutana na Aston Villa mwishoni mwa juma hili katika uwanja wao wa Vitality Stadium.