Makala

Wakora wanaotumia walemavu kusajili biashara kukwepa ushuru wawindwa Mlimani

March 8th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MAAFISA wa usalama eneo la Mlima Kenya wamezindua msako dhidi ya wafanyabiashara wanaosemekana kutumia walemavu kusajili biashara zao ili kuhepa kulipa ushuru.

Katika sheria za nchi za kuchunga masilahi ya walemavu, hawapaswi kutozwa ushuru wa biashara zao, bora tu wawe wamejiandikisha na muungano wa walemavu (PLWD).

Isitoshe, sharti wawe na cheti cha ukaguzi kuthibitisha hali yao.

Maafisa wa kiusalama wakiongozwa na Kamishna Mshirikishi wa eneo la Kati, Fred Shisia, wamesema kwamba “tunatilia mkazo kwamba kuwe na uadilifu katika kuweka ombi la kukwepa ushuru kwa kuwa mwanya huu wa kutumia walemavu kutekeleza ukora wa ukwepaji ushuru tutauziba”.

Alisema kwamba baadhi ya makateli wanatumia majina ya walemavu waliosajiliwa kutuma maombi ya kuzindua biashara, hivyo basi kukwepa ushuru kwa njia haramu.

Katika Kaunti ndogo ya Murang’a Kusini, Naibu Kamishna Gitonga Muriungi alisema kwamba wakipata leseni inayohusu mlemavu, ni lazima waombe kukutana naye binafsi.

“Tunafanya tathmini ili kubaini ikiwa mtu huyo anamiliki biashara hiyo au la,” akasema Bw Muriungi.

Alisema kwamba wawekezaji wanaoishi na ulemavu hawana cha kuogopa kwa kuwa watadumishiwa haki zao zote, na hakuna yeyote atakayewashinikiza wafunge au waanze kulipia ushuru biashara zao.

Alitumia kisa ambapo biashara kama tano tofauti zimeandikishwa kwa kutumia jina la mtu mmoja ambaye ni mlemavu, ila mwekezaji haonekani akiangazia ushahidi wa kuwa mwenye hizo biashara.

Naye Kamanda wa polisi Ruiru, Alexander Shikondi anasikitikia walemavu kutumika na mabwanyenye kumiliki biashara ilhali wanaishi masiha ya ufukara.

“Unakumbana na kisa ambapo mlemavu fulani hata ana baa, hoteli na kiwanda lakini nyumbani anaishi maisha ya umaskini mkubwa,” akasema Bw Shikondi.

Alisema kwamba hali hiyo itapigwa msasa kubaini ni jinsi gani mlemavu wa umri wa miaka kama 70 anasemwa kusajili biashara kama tano zinazoingiza faida ya mamilioni kila mwaka ilhali kila mwisho wa mwezi unampata katika foleni ya pesa za wazee akiwa anaonyesha ukata mkuu.

Naibu Kamishna Tarafa ya Maragua Joshua Okello, alisema makateli humwendea mlemavu na kumuomba stakabadhi zake za kujitambulisha na hatimaye kusajili biashara.

Alisema njama hiyo huwa na ushirika wa madalali, maafisa wa kutoa leseni hasa wa serikali za kaunti na hata wengine walio katika afisi za kutoza ushuru wa kitaifa.

“Mlemavu huyo anapewa pesa kidogo akiahidiwa kuwa atakuwa akitunzwa kila mwezi lakini baada ya muda mfupi anatelekezwa na kuachwa kwenye mataa huku mwekezaji huyo akizidi kuvuna faida kwa kuhepa ushuru,” akasema Bw Okello.

Bw Okello alionya kwamba “tukiingia katika biashara yako na tupate leseni yako ni ya mlemavu, hatutatoka hapo bila kuthibitisha”.

“Tutahitaji kuona picha yako ya kitambulisho na iwe ni yako, jina liwe ni lako na kwa uhakika iwe wewe ndiye unavuna faida na manufaa ya kukwepa kulipia ushuru kwa njia halali,” akaonya.

Mshirikishi wa muungano wa walemavu Kaunti ya Murang’a Damaris Irungu alikiri kwamba sakata hiyo imekuwa ikivumishwa na wengi.

“Sio tu katika biashara mitaani… Kuna wengi ambao hata wanaagiza bidhaa kutoka nje ya nchi wakiwa na nembo ya PLWD na kukosa kulipa ushuru. Kunafaa kuwe na mikakati maalum kuzima njama hiyo ya kutumia utapeli ili kujipa faida kwa kutumia ulemavu wetu,” akasema Bi Irungu.

Bi Irungu alisema kwamba mwanya huo wa kutumia walemavu umekuwa ukitumiwa visivyo na wengi.

Alisema kwamba wote wanaofaa kulipa ushuru wanapaswa kukabiliwa ili wasikwepe kupitia kuiga ulemavu “kwa kuwa hata sisi walemavu tunahitaji serikali iwe na pesa za kutufanikishia maisha yetu pamoja na wengine wanyonge nchini”.

[email protected]