Habari

Wakristo sasa wafanya ibada milimani na mapangoni kisiri

April 12th, 2020 2 min read

Na TITUS OMINDE

BAADA ya serikali kupiga marufuku ibada katika makanisa na mikutano ya kidini kama njia moja ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona, imefichuka kwamba baadhi ya waumini sasa wameamua kukongamana na kuendeleza maombi katika milima na mapango kisiri.

Maombi haya ya faragha yanaendeshwa kwa zamu miongoni mwa madhehebu mbalimbali katika maeneo ya Magharibi na Rift Valley.

Baadhi ya wale ambao wanaendesha maombi hayo walijitetea kwamba wanaiga Yesu Kristo, ambaye Biblia inasema alienda mlimani kuomba na kufunga kwa ajili ya uponyaji na kupata nguvu zaidi za kukabiliana na nguvu za maovu.

“Nimeamua kuendeleza maombi hapa mlimani kama alivyofanya Yesu ili kutafuta uponyaji kutokana na janga hili la virusi vya corona,” alisema Bw Joseph Kiptoo, ambaye huendesha maombi yake katika Mlima wa Kapsoya mjini Eldoret.

Bw Kiptoo alisema hatua hiyo haipaswi kuchukuliwa kama kukaidi agizo la serikali, bali ichukuliwe kama moja ya ambazo Wakristo wanatumia kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya virusi hivyo.

Mtindo huu wa kwenda kinyume na masharti ya serikali umefichuka wakati ambapo baadhi ya viongozi wa kidini wanashinikiza serikali kulegeza masharti kuhusu marufuku ya kukongamana makanisani, na katika sehemu nyingine za ibada.

Mnamo Ijumaa, wahubiri watatu waliishtaki serikali wakitaka mahakama iondoe agizo hilo, na badala yake kuwepo mwongozo utakaohakikisha waumini hawajiweki katika hatari ya kuambukizana corona wakiwa makanisani.

Hali sawa na hiyo ya maombi ilionekana katika Mlima wa Maili Nne katika Kaunti ya Uasin Gishu, ambapo waumini wa madhehebu tofauti ya Ukristo wamejificha mapangoni na vichakani wakiomba.

Unapofika katika mlima huu kile unachosikia ni watu wengi wakiomba kwa sauti za juu.

Wale ambao wanafika katika mlima huu ambao unamilikiwa na Kanisa la IVC mjini Eldoret, wanasisitiza kwamba wamezingatia masharti yote ya kujikinga na virusi kwani kuna maji ya kunawa mikono, sanitaiza, na dawa za kuua viini, na sabuni katika lango la kuingia mlimani humo.

Katika Mlima wa Likuyani maarufu kama Likuyani Prayer Mountain katika Kaunti ya Kakamega, hali ni sawa na hiyo ambapo Wakristo kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kaunti Ndogo ya Likuyani, Kakamega Mjini, Trans Nzoia na kaunti jirani ya Uasin Gishu hukusanyika kwa maombi.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Wakristo hao waliomba serikali kutoingilia hatua ambazo wanachukua kuendeleza maombi ya faragha kwani wanasema maombi yao ni kwa lengo la kukabiliana na janga la corona ambalo linakumba ulimwengu wote.

“Silaha ambayo tuko nayo kama Wakristo ni maombi. Serikali isitufuate msituni tunampotafuta Mungu ili atupiganie katika janga hili,” akasema mmoja wa waumini hao ambaye aliomba asitajwe jina.

Aliendeleai kusema kuwa, mbali n maombi ya faragha, wao wanazingatia sheria za afya ya umma katika vita dhidi ya janga hilo.

Waliahidi kuzingatia kanuni zote zilizowekwa na serikali katika vita dhidi ya virusi vya corona.

Serikali iliagiza kufungwa kwa makanisa, misikiti na maeneo mengine ya ibada mwezi jana katika jitihada za kuzuia ueneaji wa ugonjwa huo uliozuka nchini China mwaka jana.

Pia imeweka kafyu ya usiku kote nchini, kufunga maeneo ya burudani na kuweka marufuku ya kuingia na kutoka kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale ambazo zinaongoza kwa idadi ya juu ya visa vya virusi hivyo.

Kufikia jana watu 191 walikuwa wamethibitishwa kuugua ugonjwa huo hapa nchini, 24 kati yao wakitangazwa kupona.

Ugonjwa huo umesambaa katika mataifa 210 kote duniani, ambapo watu zaidi ya milioni 1.7 walikuwa wameambukizwa kufikia jana na elfu 103 kati yao kufariki.

Maradhi hayo yamelemea zaidi mataifa ya Uropa na Amerika, ambayo kufikia jana kulikuwa na watu nusu milioni walioambukizwa na elfu 18 kufariki.