Habari Mseto

Wakristo wahimizwa waombe Kenya iwe nchi ya amani

January 1st, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKRISTO wamehimizwa kumuomba Mungu ili amani idumu Kenya mwaka huu wa 2020 na raia na wageni wadumishe utangamano.

Padri Peter Maingi kutoka parokia kuu ya Nyeri, alisema kila Mkristo anastahili kutafakari mwelekeo wake na kuhakikisha anampenda mwenzake.

“Huu ni mwaka wa kutoa maamuzi ya mafanikio wala sio ya chuki. Kila mmoja anastahili kuwa na azimio lake litakalomfaa katika siku zijazo,” alisema Padri Maingi.

Alisema watu wanastahili kuwa na familia iliyo na amani na kumuogopa Mwenyezi Mungu katika vitendo vyao.

“Sisi kama Wakristo hatustahili kutembea gizani bali ni vyema kumgeukia Mungu ili aweze kutupa hekima ya kuamua mambo mema maishani.

Aliwahimiza Wakristo kufuata mienendo ya hayati Mahatma Gandhi wa India ambaye wakati wake wa uhai alifuata mwenendo wa Ukristo kwa kuhubiri kuwepo haki kwa kila binadamu, hata ingawa hakulelewa katika misingi hiyo ya Ukristo.

Aliyasema hayo katika Kanisa Katoliki la St Dominic mjini Thika, usiku wa kufunga mwaka wa 2019 na kuukaribisha mwapa 2020.

Aliwashajiisha Wakristo waombe ili nayo nchi ya Somalia – taifa jirani la Kenya – liwe na amani ya kudumu pamoja na bara la Afrika kwa jumla.

Alisema Wakristo wanastahili kuonyesha imani yao kwa vitendo.

“Wakati huu ndipo tunastahili kuombea wote wasiojiweza kifedha ili wawe na mafanikio. Tunaelewa kuna watu wengi kule nje ambao wangetamani kusherehekea mwaka mpya kwa furaha lakini hawana namna,” alieleza Padri Maingi.

Aliwahimiza Wakristo kuvumiliana hasa wakati kama huu wananchi wanapitia hali ngumu aghalabu kiuchumi.

Aliwatakia kila mmoja maisha mazuri kwa maelewano katika mwaka huu mpya wa 2020.

Alikashifu viongozi wanaojihusisha na ufisadi akisema umelemaza uchumi wa taifa.

“Sisi Wakenya tunastahili kuwa na maadili mema ili kuwa na nchi ya kutamanika na wote. Tuwe Wakristo wa kuaminika katika matendo yetu,” alikariri Padri Maingi.

Alisema Papa Francis ataiombea dunia ili kuwe na amani ya kudumu.

“Tunaelewà jinsi nchi nyingi ulimwenguni zinavyopitia wakati mgumu kwa misukosuko ya vita, njaa, na wakimbizi,” alisema mchungaji huyo Mkatoliki.