Wakristo wakosa mbwembwe za Pasaka corona ikiwafungia

Wakristo wakosa mbwembwe za Pasaka corona ikiwafungia

Na AFP

MAMILIONI ya Wakristo kote duniani jana walijiandaa kwa wikendi nyingine ya Pasaka chini ya masharti makali kufuatia ongezeko la visa vya msambao wa virusi vya corona.

Kumeripotiwa ongezeko la maambukizi katika mataifa mbalimbali ulimwenguni huku shughuli za utoaji chanjo zikishika kasi haswa katika mataifa ya Uropa.

Kupanda kwa idadi ya maambukizi kumechangaia mataifa kadhaa kuweka vikwazo zaidi kudhibiti hali hiyo, licha ya pingamizi kutoka kwa raia.Italia ilitangaza amri ya kutotoka nje kote nchini humo jana ikihofia ongezeko la maambukizi ya corona wakati wa Pasaka ambapo familia hukutana kusherehekea.

Katika Vatican, makao makuu ya Kanisa Katoliki watu wachache walitizama wakati ambapo Papa Francis alikuwa akiongoza sherehe ya “Njia ya Msalaba” katika uwanja wa St Peter Square mbele ya Kanisa la St Peter’s Basilica ambapo hapakuwa na watu siku ya Ijumaa Njema. Masharti ya Covid-19 yalizuia waumini kukongamana kwa mwaka wa pili, mtawalia.

Masharti mapya ya kuzuia maambukizi ya corona pia yaliwekwa nchini Ufaransa, huku serikali ikijizatiti kupambana na ongezeko la visa vya maambukizi ambalo limechangia hospitali kulemewa jijini Paris.

Masharti kama hayo tayari yalikuwa yamewekwa katika mataifa mengine ya Uropa kama vile Ubelgiji na Ujerumani. Chansela Angela Merkel wa Ujerumani alitoa wito kwa raia kukoma kufanya mikutano na sherehe mbalimbali msimu huu wa Pasaka.

“Madaktari na wauguzi wanafanya kila wawezalo kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19,” Merkel akasema Ijumaa, akionya kuwa hospitali zinaendelea kujaa wagonjwa wenye umri wa chini.

“Hatufai kuwatelekeza lakini tuwasaidie kwa kuchukua hatua zinazohitajika. Hii ina maana kuwa tuadhimishe Pasaka kwa utulivu; tupunguze mtagusano wa watu,” kiongozi huyo akasema.Nchini Canada marufuku kama hizo ziliwekwa kabla ya Pasaka katika mikoa ya Ontario na Quebec ambayo ndiyo yenye idadi kubwa ya watu nchini humo.

Lakini dalili za kurejelewa kwa hali ya kawaida zilionekana Mji wa Kale wa Jerusalem, Israel ambako marufuku ya Covid-19 ilivuruga Pasaka mwaka jana.Mwaka huu makundi ya watu wachache yalionekana huku vituo kadhaa vikifunguliwa.

Hii inatokana na ufanisi ambao umeandikishwa na Israeli katika utoaji chanjo ya Covid-19.“Mwaka jana, mambo yalikuwa magumu. Tulihisi kana kwamba jiji lilifungwa,” akasema Lina Sleibi, Mpalestina mmoja Mkristo ambaye huimba kwenye ibada za kanisa katika mji wa Bethlehem ulioko West Bank.

“Sasa tunahisi kwamba umepata uhai mpya,” akasema.Janga la Covid-19 limeua zaidi ya watu 2.8 milioni duniani kufikia jana, idadi ambayo inaendelea kuongezeka.

You can share this post!

Maseneta wakosoa Joho kuhusu matumizi ya feri

Chanjo ya AstraZeneca yaua watu saba