Makala

Wakulima 1,000 waungana kutumia viazi vitamu kuoka mikate

September 3rd, 2020 3 min read

Na PETER CHANGTOEK

WAKULIMA wanaovikuza viazi vitamu katika eneo la Maua, Kaunti ya Meru, wana kila sababu ya kutabasamu, maadamu watanufaika kutoka kwa uongezaji wa thamani kwa mazao yao.

Hii ni kwa sababu kuna kiwanda kimoja ambacho kiliasisiwa ili kuongeza thamani kwa mazao ya viazi vitamu. Kiwanda hicho kiliasisiwa na wakulima zaidi ya elfu moja, na huutumia unga wa viazi vitamu kutengeneza bidhaa kumi na moja, ikiwemo mikate.

Bidhaa zizo hizo zimeidhinishwa na Shirika la Kukagua Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS). Baadhi ya bidhaa hizo ni: mikate, keki zijulikanazo kama ‘queen’, donati (doughnuts) na kaukau (crisps).

Lakini je, kiwanda kiki hiki kilianzishwa linin na vipi? Katika utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo mwaka 2010, ilibainika kuwa katika nyanda za chini katika Kaunti ya Meru, mabadiliko ya hali ya hewa na umaskini ulikuwa wa hali ya juu mno, kiasi cha kuwanyima wenyeji afya njema.

Baada ya mjadala pevu kuhusu zao ambalo lingeweza kuimarisha afya na maisha ya wenyeji wa eneo hilo, mmea uliopendekezwa ukawa ni viazi vitamu wenye rangi ya njano ndani.

Julius Inyingi, mwenyekiti wa chama cha ushirika kijulikanacho kama Meru Friends Sacco, kinachoziendesha shughuli katika kiwanda hicho, anadokeza kuwa kiangazi kilikuwa kikichangia mno kuwapo kwa ukosefu wa lishe.

“Ukosefu wa mvua ya kutotegemewa ulisababisha kiangazi, na kuweka eneo hili katika hatari ya kukosa lishe za kutosha,” afichua mwenyekiti huyo, akiongeza kuwa hilo liliwafanya watoto wengi kutoenda shuleni kwa kukosa vitamini pamoja na madini muhimu yanayotakiwa kwa ajili ya kukua kwa watoto, na hivyo kuathiriwa na maradhi kwa urahisi.

FELIX Juma, mhudumu akionyesha baadhi ya mikate iliyookwa kwa kutumia unga wa viazi vitamu, katika kiwanda chao kule Maua, Kaunti ya Meru. PICHA/ PETER CHANGTOEK

Ili kulitatua tatizo lilo hilo, ukulima wa viazi vitamu ukapewa kipaumbele kwa wanaoishi katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Inyingi, mmea wa viazi vitamu aina ya Orange Red Fleshed, ukapewa kipaumbele kukuzwa katika eneo hilo kwa sababu zao hilo lina vitamini A, madini kadhaa k.v chuma na ‘potassium’.

Kiwanda hicho kiliasisiwa mnamo mwaka 2018. Hata hivyo, wakulima waliopewa kandarasi ya kuukuza mmea huo, wakashindwa kuyazalisha mazao ya kutosha kukiendesha shughuli kiwandani.

Ili kukiwezesha kiwanda hicho kuendeleza shughuli zake vyema, wakulima walipewa matagaa bora ya viazi vitamu ili kuyakuza.

Matagaa hayo, ambayo hustahimili kiangazi, magonjwa na huwa na virutubisho muhimu, yalizalishwa katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kaguru (Kaguru Agricultural Training Centre). Kituo hicho cha kilimo kiko chini ya idara ya zaraa, katika Kaunti ya Meru.

Kwa madhumuni ya kuwakinga wakulima dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa, wakulima hao hao walishauriwa kuvikuza viazi vitamu kwa mashamba makubwa makubwa.

Kwa kuwa eneo la Meru lina joto, viazi vitamu hukua upesi, maadamu mmea huo hukua vyema katika maeneo yenye joto.

Ili kuwashawishi wakulima kuvizalisha viazi vitamu kwa wingi, Inyingi anafichua kuwa mmea huo hauchukui muda mrefu sana ili kukomaa, na huweza kukuzwa kila wakati.

Mradi uo huo umeanza kuwasaidia wakulima kwa hali na mali, ambao wanaishi katika kaunti-ndogo tisa zilizoko kule Meru, ambao wamekuwa wakiyauza mazao yao ya viazi vitamu kwa bei duni.

Awali, wakulima wa viazi vitamu walikuwa wakipunjwa na madalali, ambao walikuwa wakivinunua viazi vitamu kwa bei ya Sh2,000 kwa gunia kubwa la uzani wa kilo 80. Hilo kwa sasa limezikwa katika kaburi la sahau, kwa sababu wakulima huyauza mazao yao kwa kiwanda hicho.

Baada ya kuviwasilisha viazi vitamu kwa kiwanda hicho, wao hulipwa kabla siku saba hazijaisha, ambapo wao hulipwa Sh50 kwa kilo moja ya mazao hayo.

Mradi huo ulifadhiliwa na Halmashauri ya Kitaifa ya Kukabiliana na Kiangazi (NDMA) na Muungano wa Ulaya (EU).

“Viazi vitamu vinaweza kuchemshwa, kuokwa, kuchomwa au hata kuliwa vikiwa vibichi….,” asema Inyingi.

Kiwanda hicho kinalenga kupunguza hali ambapo jamii hutegemea ufadhili kutoka kwa wafadhili. Aidha, husaidia kupunguza njaa na huwapa vijana na wanawake ajira.

Kwa mujibu wa Hellen Ringera, mwanalishe katika Kaunti ya Meru, ni kwamba, mbali na kuwapa wenyeji lishe, mradi huo pia utawafaa kwa mafao makubwa wakulima kupata riziki.

Anaongeza kuwa mradi huo utawapa ajira wenyeji, na kurefusha muda wa mazao kupitia kwa uongezaji wa thamani kwa viazi vitamu.