Habari

Wakulima 12,000 Kwale wafaidika na mashine za kupukuchua mahindi

September 7th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

WAKULIMA 12,000 katika Kaunti ya Kwale wamefaidika na mashine za kupukuchua mahindi na miche iliyoboreshwa zilizotolewa na serekali ya kaunti hiyo.

Mashine hizo zinapangiwa kuwapunguzia wakulima muda wa kutayarisha zao hilo kwa usagaji wa unga.

Naibu gavana wa kaunti hiyo Bi Fatuma Achani alisema mashine hizo zitagawanywa katika wadi 20 katika kaunti hiyo na zitawasaidia wakulima 625 katika wadi hizo.

Aidha alisema kilo nane za miche mbalimbali ya vyakula zitagawanyiwa kila mkulima katika kaunti hiyo.

“Hatua hii ni kuongeza mazao ya chakula katika kaunti yetu ili kudhibiti makali ya njaa na kuimarisha kilimo kwa kuwapa wakulima mazingira bora na usaidizi ufaao,” akasema.

Alisema mashine hizo zina uwezo wa kupukuchua mahindi na pojo ambayo ni mazao maarufu katika eneo hilo.

Akizungumza katika mtaa wa Patanani Matuga, Bi Achani alisema serikali ya kaunti hiyo imeanzisha mradi huo kuwasidia wakulima wadogo wadogo ili kuwainua.

Aliongezea kusema kuwa kaunti hiyo itahakikisha kuwa wakulima wanapata maji ya kunyunyuzia mimea yao na matingatinga ya kulima.

“Tunafanya hivi ili kuhakikisha Kaunti ya Kwale inajitegemea kwa kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi yao na pia kuuza kwa kaunti nyengine,” akasema.

Alisema kuwepo kwa matingatinga, dawa za kuuwa wadudu, mbolea na maji kutawasukuma wakulima wengi ambao hawakuwa na uwezo wa kupata vifaa hivi kuingia kilimobiashara; hatua ambayo itaboresha hali ya maisha ya wenyeji katika eneo hilo.