Habari Mseto

Wakulima ambao ardhi zaozilitwaliwa kwa ujenzi wa kiwanda cha Sh21 bilioni cha nishati ya upepo wataka Rais Kenyatta kuwasaidia kusuluhisha utata

November 5th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

WAKULIMA wanaomiliki mashamba yaliyotwaliwa kufanikisha ujenzi wa kiwanda cha nishati ya upepo, Kaunti ya Lamu sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kusuluhisha utata unaozingira mradi huo.

Mradi huo wa gharama ya Sh 21 bilioni ulinuiwa kujengwa katika kijiji cha Baharini, mfadhili mkuu akiwa ni kampuni ya Elicio kutoka Ublegiji kwa ushirikiano na Kenwind Holdings Limited ya humu nchini.

Tayari jumla ya ekari 3,206 za ardhi zilitwaliwa eneo la Baharini ili kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho kinachotarajiwa kuzalisha megawati 90 za umeme punde kitakapokamilika.

Mnamo Julai mwaka huu, Bunge la Kaunti ya Lamu lilipitisha mswada wa kuutupilia mbali mradi huo kwa kigezo kuwa mwekezaji alikiuka matakwa yaliyowekwa, ikiwemo kuwafidia wamiliki wa ardhi husika kwa wakati uliopangwa.

Katika mahojiano na wanahabari kijijini Baharini Alhamisi, wamiliki wa mashamba husika walimuoimba Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kutatua mzozo uliopo ili mradi huo uendelee kujengwa eneo lao.

Wakiongozwa na Msemaji wa Wakulima wa Baharini, Linus Gachoki, walisema hatua ya madiwani wa Bunge la Lamu ya kutupilia mbali mradi haifai.

Bw Gachoki aliwakashifu madiwani hao kwa ubinafsi ambao umepelekea wakulima kubaki wakihangaika bila fidia walizotarajia kutoka kwa mwekezaji wa kiwanda hicho.

“Tunaomba serikali kuu kupitia Rais wetu, Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kusuluhisha utata uliokwamisha mradi. Tunahitaji mradi uendelee ili tupate kulipwa fidia zetu za ardhi. Sisi hatujakuwa na tofauti zozote na mwekezaji,” akasema Bw Gachoki.

Joseph Mwangi ambaye ni mmoja wa waathiriwa waliotwaliwa mashamba yao kufanikisha ujenzi wa mradi huo wa nishati ya upepo alisema mbali na fidia, mwekezaji pia alikuwa ameahidi mambo mengi mazuri kwa jamii ya eneo la Baharini.

Kama njia mojawapo ya kuendeleza ushirikiano mwema kwa jamii, mwekezaji alikuwa ametangaza mpango wa kutenga Sh 40 milioni kama hazina itakayoinua jamii ya Baharini hasa iwapo mradi huo ungefaulu kuanzishwa Lamu.

“Sh 40 milioni zingeshughulikia ujenzi wa shule na zahanati. Pia zingetumika kusomeshea watoto wetu. Vijana hapa pia wangepata ajira kwenye mradi huo. Hii inamaanisha haya hatutayapata kwani madiwani wetu wametupilia mbali mradi kwa sababu zao za kibinafsi. Rais asikie kilio chetu na kutatua utata uliopo,” akasema Bw Mwangi.

Bi Mary Kimani alitaja kutupiliwa mbali kwa mradi huo kuwa pigo kwao kwani wengi wao tayari walikuwa wamefanya mipango na kukopa fedha kutoka kwa benki na mashirika mengine, wakitarajia kuwa fidia watakayopata wangetumia kulipa mikopo hiyo.

Bi Kimani alieleza kusikitishwa kwake na hatua ya madiwani ya kutupilia mbali mradi, hivyo kukosesha matumaini ya wamiliki wa ardhi husika kufidiwa.

“Tumesubiri fidia zetu kwa karibu mwongo mmoja sasa. Wametupilia mbali mradi ilhali sisi tulikuwa na matumaini mengi kwamba ardhi zilizotwaliwa kufanikisha mradi huo zingefidiwa. Mamilioni yote tuliyotarajia sasa yameenda hivyo,” akasema Bi Kimani.