Wakulima Kiambu wapokea hundi ya Sh39 milioni kupiga jeki shughuli zao za kilimo

Wakulima Kiambu wapokea hundi ya Sh39 milioni kupiga jeki shughuli zao za kilimo

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI ya Kaunti ya Kiambu imetoa hundi ya Sh39 milioni kwa wakulima ili waimarishe shughuli zao za kilimo.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, alisema hatua hiyo ni njia mojawapo ya kuwapa wakulima hao mwelekeo wa jinsi ya kupanda chakula na kukihifadhi kiwe cha manufaa hata kipindi cha kiangazi na njaa.

Wengi wa wakulima hao ni wale wanaohusika na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, kuku, viazi, ndizi, na mahindi.

Wakulima hao wanatoka maeneo ya Kikuyu, Limuru, Gatundu Kusini kaskazini, na Lari.

“Kuna haja ya wakulima kupewa mawaidha ya jinsi ya kutumia fedha hizo kwa lengo la kuimarisha kilimo chao. Wakulima hao waliojumuika mjini Kiambu leo Jumatatu watapata hamasisho la jinsi ya kujisimamia kwa kuzingatia kilimo bora,” alifafanua Dkt Nyoro.

Alisema maafisa wa kilimo kutoka Kaunti ya Kiambu watakuwa wakiwatembelea wakulima hao ili kuwapa motisha na matumizi ya teknolojia ya kisasa.

” Tunataka kuona wakulima kutoka kaunti hii ya Kiambu wakipata mazao ya kutosha huku pia wakiendesha ufugaji kwa njia ifaayo,” alieleza gavana huyo.

Alisema wakulima hao walihimizwa kuzingatia kutumia mbolea ya kisasa ili kuongeza mapato zaidi kwenye kilimo chao.

Alisema maafisa wa kilimo watakuwa na jukumu la kuwatembelea wakulima hao kila mara ili kujua shida wanazopitia ili wazitatue mara moja.

“Tungetaka kuona wakati wa mavuno kila mkulima anajivunia kutokana na kile amepanda. Kwa hivyo ninamshauri kila mmoja achukulie mpango huo kwa uzito na aupe zingatio zaidi. Tungetaka kuona Kaunti ya Kiambu ikiwa ndiyo inakuwa kama ghala la kusambaza chakula kwingineko,” alishauri wakulima hao.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wataalam wa kilimo, na maafisa wakuu kutoka kaunti hiyo.

Ili kufanikisha mpango huo wakulima hao walishauriwa kujiweka kwa makundi.

You can share this post!

Familia zaidi ya 50 zapoteza nyumba zao kwenye mkasa wa moto

Utata zaidi kuhusu mustakabali wa Messi kitaaluma Barcelona...