Habari Mseto

Wakulima kuuza kahawa Amerika

March 7th, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

WAKULIMA wa kahawa katika Kaunti ya Kirinyaga, huenda wakapata afueni baada ya soko jipya la kuuza bidhaa zao kupatikana nchini Amerika, kulingana na Gavana Anne Waiguru.

Gavana Waiguru aliambia Kongamano la Ugatuzi linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Kirinyaga, kuwa serikali yake tayari imepata ghala la kuhifadhi kahawa nchini Amerika.

Bi Waiguru alisema kuwa eneo hilo linaongoza katika uzalishaji wa kahawa yenye ubora wa juu.

“Tutakuwa tukiuza nchini Amerika kati ya tani nne na tano za kahawa kwa wiki.

Alisema wakulima wataanza kuuza kahawa yao kwa kati ya Sh100 na Sh120 kwa kila kilo, mazao yao yakianza kuuzwa katika soko hilo jipya.

Wakulima wamekuwa wakiuza kahawa yao kwa bei duni na malipo yao hucheleweshwa.

Ikiwa mpango huo wa kuuza kahawa nchini Amerika utafaulu, basi huenda ikawa afueni kwa wakulima hao.

“Kwa sasa tunauza kahawa kwa Sh50 kwa kila kilo ya kahawa. Tunafurahi kwamba serikali ya kaunti imetutafutia soko ambalo huenda likatuongezea mapato,” akasema Muriuki Njoka ambaye ni mkulima.

Bi Waiguru alisema serikali yake itahakikisha kuwa wakulima ambao wamekuwa wakihangaika kuuza mazao yao wanapata faida.

Gavana aliambia kongamano kuwa kaunti yake inaongoza katika uzalishaji wa mchele katika eneo la Mlima Kenya na kuna mipango ya kujenga kiwanda katika eneo la Mwea.