Wakulima sasa wauza mahindi yao nje ya nchi

Wakulima sasa wauza mahindi yao nje ya nchi

Na BARNABAS BII

WAKULIMA katika eneo la North Rift sasa wanauza mahindi yao katika mataifa ya Sudan Kusini, Kaskazini mwa Uganda na Rwanda kutokana na ongezeko la hitaji la zao hilo.

Hali hiyo imechangia wakulima hao kuuza mahindi yao kwa bei nzuri.

Huku Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) ikinunua mahindi ya wakulima kwa bei ya Sh2,400 kwa gunia moja la kilo 90, wakulima wanalipwa Sh2,900 wakiuza nje ya mpaka.

Kulingana na ripoti kuhusu uzalishaji wa mahindi katika kanda ya North Rift, bei ya mahindi inatarajiwa kuendelea kupanda kwa sababu ya hali mbaya ya anga iliyoathiri mimea ya mahindi.

Vile vile, bei itapanda kulingana na mapigano yanayoshuhudiwa katika mataifa ya Ethiopia na Sudan Kusini.“Bei ya mahindi yako juu kaskazini mwa Uganda na Rwanda kutokana na ongezeko la hitaji.

Hii ni licha ya kufunguliwa kwa mpaka wa Uganda na Rwanda, hali ambayo imechangia kuimarika kwa biashara ya mahindi,” ikasema ripoti kwa jina Famine and Earliy Warning System Network ya Septemba 2021.

Kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) hali ya ukame imeathiri uzalishaji wa mimea ya chakula katika maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Uganda. Hali hiyo imechangia kupungua kwa viwango vya mafuno.

“Uhaba wa mvua ya kutosha umechangia kunyauka kwa mimea ya mtama na mahindi, hali ambayo imeathiri viwango vya mavuna,” ikasema ripoti hiyo.

Muungano wa Kampuni za Usagaji Nafaka (GBMA) unaoleta pamoja zaidi ya kampuni 35 ndogo za usagaji, Alhamisi ulionya huenda bei ya mahindi nchini ikapanda zaidi kwa sababu wakulima wengi wanaamua kuuza mazao yao nje ya nchi.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU

Ramaphosa afokea mataifa ya Afrika yanayotenga Afrika Kusini

T L