Habari za Kaunti

Wakulima Taita Taveta kujinyanyua na mbolea nafuu, upimaji udongo

February 23rd, 2024 2 min read

NA LUCY MKANYIKA

KATIKA miaka ya awali, Kaunti ya Taita Taveta ilikuwa ikilisha eneo la Pwani na maeneo mengine, kwa kutoa mazao safi kwa masoko ya Mombasa na Nairobi.

Hata hivyo, kaunti hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uzalishaji mdogo wa mazao, udongo kuharibika, na gharama kubwa za pembejeo, zinazoathiri maisha ya maelfu ya wakulima.

Hata hivyo, msimu huu, wakulima wana sababu ya kutabasamu, kwani wamepata mavuno mengi, baada ya mvua kubwa iliyoshuhudiwa katika eneo hilo.

Katika msimu ujao, wakulima wanatarajia kunufaika na upimaji wa udongo bila malipo na mbolea ya bei rahisi, kama juhudi za serikali za kuimarisha uzalishaji na usalama wa chakula katika kaunti hiyo.

Upimaji wa udongo husaidia wakulima kubaini aina na kiasi sahihi cha mbolea ya kutumia, ili kupata mazao bora katika udongo mbalimbali.

Hata hivyo, wakulima wengi katika kaunti hiyo hawajaweza kupata huduma hizo kutokana na changamoto, zikiwemo gharama kubwa, ukosefu wa habari, vifaa na maabara ya kupima.

Mkulima John Mwamburi aliambia Taifa Leo kuwa licha ya kuwa mkulima kwa zaidi ya miaka 20, hajawahi kupima udongo wa shamba lake.

“Ninatumia mbolea ile ile kila msimu nikitarajia mavuno mazuri. Wakati mwingine napata mavuno mazuri lakini wakati mwingine huwa naambulia patupu. Sijui nini kibaya na udongo wangu,” akasema Bw Mwamburi ambaye anafanyia shughuli zake za kilimo katika kijiji cha Werugha.

Wakulima wengi katika kaunti hiyo hubahatisha au kutafuta ushauri kutoka kwa wakulima wenzao wakati wa kutumia mbolea bila kujua viungo vinavyohitajika kwa udongo wao.

Uzinduzi wa mbolea ya bei nafuu mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta. Kila gunia ni Sh2,500. PICHA | LUCY MKANYIKA

Aidha, wakulima hao hawana habari kuhusu aina na wakati unaofaa wa kuweka mbolea ili kuongeza mavuno yao na hivyo kusababisha uzalishaji mdogo, afya duni ya udongo, na uharibifu wa mazingira.

Akizungumza mjini Voi wakati wa kutoa mbolea kwa wakulima, Afisa Mkuu wa Kilimo wa kaunti hiyo Bw Steven Mcharo alisema serikali imetambua tatizo hilo na imechukua hatua za kukabiliana nalo kupitia Mradi wa Kitaifa wa Maendeleo ya Thamani ya Kilimo (NAVCDP).

Mpango huo wa kitaifa unaolenga kutoa upimaji wa udongo na huduma za ushauri kwa wakulima wadogo nchini kote unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kutekelezwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika kwa ushirikiano na serikali za kaunti.

Bw Mcharo alisema mradi huo unatarajiwa kuanza Machi, ambapo kutakuwa na zaidi ya maabara 2,341 ambapo wakulima watapeleka sampulo za udongo wao kupimwa bila malipo yoyote.

“Mradi utaanza wiki ijayo. Wakulima watapata matokeo ya udongo wao mara moja ili kuwasaidia kuuboresha na kuongeza uzalishaji wao,” alisema.

Alisema mradi huo utasaidia wakulima kuboresha udongo na mavuno ya mazao yao, pamoja na kupunguza gharama za pembejeo na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wakazi huohuo, zaidi ya magunia 3,000 ya mbolea yanatarajiwa kusambazwa kwa wakulima katika kaunti hiyo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Rasilimali za Habari za Kilimo kilicho chini ya Wizara ya Kilimo, Bi Philgona Ooko, alisema kuwa shehena hiyo ni mpango wa serikali kuwapa wakulima mbolea kabla ya kuanza kwa mvua kipindi cha Machi hadi Mei.

Wakulima watanunua mbolea ya bei rahisi kwa Sh2,500 kwa gunia la kilo 50.

Bi Ooko alisema mpango huo unalenga kuwakinga wakulima dhidi ya gharama kubwa za uzalishaji.

Vilevile, alifichua kuwa serikali itaanza kuchukua picha za mashamba ya wakulima na maelezo ya kibaiolojia, ili kuhakikisha wakulima halisi wanafaidika na mpango huo wa mbolea.

“Tunataka kuhakikisha kuwa ni wakulima tu wanaostahili wanaonufaika na mpango huu,” alisema.