Wakulima wa chai kulipwa bonasi ya juu mwaka ujao

Wakulima wa chai kulipwa bonasi ya juu mwaka ujao

Na DERICK LUVEGA

WAKULIMA wa majanichai sasa wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Waziri wa Kilimo Peter Munya kutangaza kuwa wataanza kulipwa bonasi za juu mwisho wa mwaka wa fedha 2021/22.

Kati ya marekebisho mapya katika sekta ya majanichai ambayo yanatarajiwa kuanza kutekelezwa, ni usawazishaji wa bei ili kukinga wakulima wakati bei ya soko la kimataifa inashuka.

Tangazo la Bw Munya lilijiri wakati ambapo serikali imesema bonasi ya mwaka 2020/21 italipwa mwezi ujao; ingawa itakuwa chini mno kutokana na bei ya chini ya zao hilo kimataifa, pamoja na usimamizi mbaya wa Mamlaka ya Ustawi wa Majanichai (KTDA).

Waziri alikuwa akizungumza katika ziara yake kwenye kiwanda cha majanichai cha Mudete, Kaunti ya Vihiga. Alisema ingawa wakulima watapokea bonasi ya sasa ya Sh6 kwa kilo – ambayo ni chini mno – mwaka ujao pesa hizo zitapanda na watafurahia jasho lao.

Kabla ya kukumbatia wazo la kusawazisha bei ya majanichai, Bw Munya alisema kuwa wakulima walikuwa wakiumia kwa kuwa bei ilikuwa ikipungua kila mara. Hali hii ilichangia baadhi ya wakulima kung’oa majanichai kisha kuanza kupanda mimea mingine.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Yashangaza mno wazee kutawaza watu kiholela

Mjumbe wa Taliban anyimwa fursa kuhutubia kikao cha UN