Wakulima wa maembe hoi kampuni  kukosa kununua zao

Wakulima wa maembe hoi kampuni kukosa kununua zao

NA MWANDISHI WETU

Kufufuliwa kwa kiwanda cha kusindika Matunda cha Galole mwaka wa 2019 kuliwapa matumaini makubwa wakulima wa maembe katika Kaunti ya Tana River.

Mamlaka ya Maendeleo ya Pwani (CDA) iliwaahidi wakulima zaidi ya 20,000 kutoka kaunti za Tana River, Lamu na Kilifi, soko la zao hilo,ila sasa imewaacha katika mahangaiko, huku mazao yao yakiozea shambani.

Mtambo huo ulifanyiwa majaribio yake ya kwanza ya kusindika maembe mwaka wa 2019, na hivyo kuwapa moyo wakulima waliojizatiti kupata maembe safi kwa ajili ya kuafikia ubora uliohitajika,ila sasa CDA imedai kuwa mazao yao ni machache,hivyo haiwezi kustahimili matarajio ya mtambo huo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu Dkt Mohammed Keinan,mtambo huo unastahiki zaidi ya tani 30,000 kwa mwaka, tani 15,000 zaidi ya kile wakulima hao wanakizalisha.

“Imetubidi kuanzisha mashamba zaidi ya miembe ya kisasa, ili tuweze kumudu utendakazi katika mtambo huo kwani mashine ile ikianza kazi haifai kupumzika,” aliielezea jarida hili.

Hata hivyo,madai hayo yamekanushwa na mhandisi mmoja katika kampuni hiyo, akisema kuwa mtambo huo umekosa kifaa muhimu kilichoharibika katika pilka pilka za kufanya majaribio zaidi,na hivyo lazima shirika ligharamike pakubwa kuagiza kifaa hicho Ulaya,ilikotengezwa mashine hiyo.

Kadri mapungufu hayo yanapozidi kuwatafuna ndimi CDA, wakulima wa maembe wanazidi kuhesabu hasara ya maelfu ya pesa huku mazao yao yakiozea shambani.

Ahadi waliyopewa na CDA iliyobashiri mwisho wa dhiki za madalali ambao walinunua embe kwa Sh2 sasa imesalia kuwa ndoto.?Utajiri walioubashiri umegeuza sura na sasa ufukara wawazomea.

Jonathan Jilo,mkulima mkongwe wa maembe katika kijiji cha Bondeni anapuzilia mbali madai ya CDA ya uhaba wa maembe kutosheleza mtambo, akimtaka mkurugenzi wa shirika hilo kutoa ushahidi wa madai hayo ama kujiuzulu.

Kulingana na Bw Jilo,ripoti ya idara kuu ya kilimo nchini inaeleza wazi uzalishaji wa maembe katika kaunti hiyo ni wa juu,huku kaunti hiyo ikiorodheshwa ya pili nchini baada ya kaunti ya Makueni, ikiwapiku na tani 200 tu.

“Mtambo huo ulikuwa wa kutuepusha na upotevu wa tani zaidi ya 20,000 za maembe, CDA ilitutia moyo, wakaturai kuongeza uzalishaji wakisema tulichonacho ni kidogo sana ukilinganisha na kile ambacho mtambo huo ulihitaji,” anasema Bw Jilo.

Kiwanda hicho kilikuwa kitengeneze tani 40,000 za sharubati kwa mwaka kwani mashine zile mpya zilikuwa na kimo kikubwa kwa mujibu wa wasimamizi wa CDA.

Kufuatia taarifa hizo, wakulima walichangamka na kuanza zoezi la kuongeza uzalishaji kwa kujitosa katika miche ya miembe iliyopandikizwa kwa nia ya kupata mavuno ya haraka.

Hata hivyo, kadri jitihada zao za mazao mapya na yenye tija zikiendelea kustawi, ndoto za kuwa na soko kwa mazao yao zinafifia siku baada ya nyingine.

“Tumepata gharama kubwa tukiwasubiri waje tuweke mkataba wa jinsi tutakavyowauzia maembe,kumbe mtambo washauua haufanyi kazi tena, wametubwaga mno,” alifoka Bw Jilo.

Huko Tana Delta, katika kijiji cha Kibusu, wakulima ambao waliasi kufanya biashara na madalali kwa matumaini ya kuuza maembe yao kwa kampuni hiyo wanahesabu hasara kubwa.

Wamebaki kutazama kwa masikitiko maembe yao yakiozea kwa shamba na maghala.

Kulingana na Bw Felix Majiba, mkulima, afisa mmoja aliyedai kuwa wakala wa CDA eneo hilo aliwaendea wakulima kutafuta miembe kwa ahadi ya kununua matunda hayo, ila baada ya wakulima hao kuvuna zaidi ya tani themanini za maembe,wakala huyo alidinda kushika simu za wakulima na kuwaacha katika njia panda.

“Waliahidi kuja ili tuhalalishe kandarasi hiyo huku wakibeba mavuno kwa msanjaa huo huo, lakini wamekataa kuchukua simu na wanaturusha huku na kule huku matunda haya yakiharibikia shambani,” alisema.?Alibainisha kuwa zaidi ya wakulima mia tatu wameathirika, na hawana mtu wa kumgeukia ili kupata msaada.

Matumaini yao katika msimu waliouona kuimarika, yametawanyika na sasa wanalazimika kukimbilia biashara zingine ili kufadhili mahitaji na majukumu yao ya nyumbani.

“Tulitarajia bora tukiwa na viwanda hivi, walikuwa wakitoa pesa nzuri zaidi ukilinganisha na wale madalali, lakini sasa wametuacha katikati ya jangwa, bila mbele wala nyuma hatujui pa kuelekea,” alisema Margaret Haboya, mkulima.?Katika kijiji cha Bondeni ,eneo bunge la Galole, wakulima wa miembe hawajakwepa shoka, soko walilotarajia limewavunja moyo na lile walilolitegemea sasa limekuja na masharti magumu.

Sasa wanalazimika kung’ang’ania kuuza kila tunda kwa shilingi moja na senti hamsini kwani madalali wamewatwisha mzigo mkubwa wa kuwalipa wavunaji na wasafirishaji kutoka shambani hadi kwenye lori.

Maisha yao yameathiriwa sana, mapato yao yamebaki kwenye michubuko na kuwaacha bila mbadala wenye tija.?Wengine wameamua kuajiri watu wa kuuza maembe hayo kwa wenyeji sokoni, huku wengine wakijadiliana na wauzaji wa sharubati za kienyeji na wauzaji pombe ili wanunue kadri wawezavyo.

Gavana wa Tana River Dhadho Godhana alitaja hali kuwa mbaya na anatamani serikali kuu ingekabidhi kiwanda cha kusindika Matunda cha Galole kwa serikali ya kaunti.

Kulingana na Bw Godhana, yeye ndiye mwanzilishi wa mradi huo alipokuwa Mbunge wa Galole, na anaweza kukifanya kiwanda hicho kuwa hai kama ilivyofikiriwa hapo awali.

“Kiwanda hiki kinaweza kutumika kikamilifu ili kuwanufaisha wakulima, lakini inaonekana hakuna nia njema ya kufanya hivyo, lakini tunatafuta masoko mengine mbadala kwa wakulima wetu wa miembe,” alisema.?Kulingana na gavana huyo, utawala wa kaunti uko kwenye msako wa masoko ya kimataifa nchini India na Sri Lanka ambayo yanaishiwa na usambazaji msimu ambao Tana River inashamiri kwa zao hilo.

Pia, Bw Godhana anadokeza kuwachukua wakulima kwa ajili ya kujifunza mbinu nyingine za kuongeza thamani ya matunda hayo.

Hata hivyo, alisisitiza wakulima kujiunga na vyama vya ushirika na kuviimarisha kwa ukuaji bora.

“Wakulima wengine nchini wanafanya uuzaji bidhaa zao kupitia Vikundi vya Ushirika, kikundi hicho kinawasaidia kujadili kama kitengo, na kutengeneza sera isiyogawanyika inayowapa faida sokoni, tatizo la wakulima wetu hawasikii kamwe,” alisema. .

Kiwanda cha kusindika Matunda cha Galole kilianzishwa mwaka 2012, kikizalisha juisi ya embe na maji ya chupa kwa ajili ya soko la kanda ya pwani.

Kutokana na ubadhirifu na ufisadi, kiwanda hicho kilianguka na kuwaacha wakulima wa miembe katika mikoni hatari ya madalali ambao walinunua maembe yao kwa Shilingi mbili kwa tunda moja ikilinganishwa na Sh20 za CDA kwa kilo.?Wakulima wengi waliamua kuuza maembe mitaani na kutengeneza sharubati za kienyeji kama njia za kuongeza thamani katika mavuno yao ya maembe, kwa nia ya kupata bei nzuri.

Hata baada ya wakulima elfu ishirini wa maembe kupata mafunzo ya uzalishaji bora wa maembe, masoko, na kuweka benki kwenye meza katika juhudi za kuwakuza wajasiriamali bora kwa hisani ya CDA, matokeo bado hayajaonekana.

  • Tags

You can share this post!

Rupia arejea nchini baada ya kukatiza mkataba Saudi Arabia

Hii hapa siri ya mbuzi kuzaa mapacha; kutoa maziwa mengi

T L