Habari Mseto

Wakulima wa majanichai Gatundu Kaskazini washabikia pendekezo la Munya

October 11th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA zaidi ya 1,000 wa majanichai katika eneo la Gatundu Kaskazini wamepitisha kwa kauli moja mapendekezo yaliyo kwenye mswada unaolenga kuboresha sekta hiyo.

Kwa kauli moja walikubaliana na mapendekezo mapya yaliyowasilishwa mbele yao na Waziri wa Kilimo na Vyama vya Ushirika Bw Peter Munya ili wayapitishe.

“Bila kuwaficha, kinachohujumu juhudi zenu nyingi wakulima wa majanichai ni mawakala ambao ajenda yao kubwa huwa ni kunyanyasa mkulima,” alisema waziri huyo.

Wakulima hao walipitisha kwa kauli moja ya kwamba wakurugenzi watakaosimamia viwanda vyao katika makundi yao watalazimika kufanya kazi kwa kipindi cha jumla ya miaka sita kwa vipindi viwili vya miaka mitatu.

“Hicho sio kiti cha kukalia milele, lakini unatakiwa uwe mtumishi wa watu waliokuchagua,” akashauri waziri huyo.

Aliwaeleza kuwa majanichai ya Kenya yanapofika katika soko la nje huwa na thamani kubwa kifedha.

Alisema wakulima wana nafasi kubwa ya kupitisha azimio la zao hilo la majanichai.

Alipendekeza kuwa kila baada ya siku 14 wakulima wanastahili kupokea marupurupu yao kutokana na chai inayouzwa kila mara katika soko la Mombasa.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa katika uwanja wa shule ya msingi ya Ndiko eneo la Gatundu Kaskazini.

Wakulima wengi waliohojiwa walikiri ya kwamba wamepitia maisha ya ufukara kwa muda mrefu kutokana na kupunjwa na mawakala.

 

Waziri wa Kilimo Peter Munya. Picha/ Lawrence Ongaro

Mkulima Peter Kamunya wa majanichai wa kutoka kiwanda cha Kagwe, Gatundu Kaskazini alisema wakulima wengi wamebaki mafukara vijijini kwa sababu wanalipwa pesa chache kabisa.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle ‘ Wainaina aliwahakikishia wakulima hao kuwa wao kama wabunge watapitisha mswada huo mpya mara moja pindi tu utawasilishwa mbele yao.

“Sisi viongozi hasa wa eneo hili tungetaka kuona mkulima wa majanichai akinufaika na jasho lake bila kunyanyaswa na mawakala,” alisema Bw Wainaina.

Aliwahimiza wakulima hao kufanya juhudi kupanda parachichi na macadamia kwa sababu mazao hayo yana soko kubwa sana katika nchi za nje.

“Nchi ya Kenya ndiyo inayoongoza kwa ukuzaji wa macadamia ulimwenguni. Kwa hivyo fanyeni bidii katika kilimo cha uzalishaji wa mazao hayo,” alisema mbunge huyo, na kuongeza “siku za hivi karibuni pia mtaweza kumiliki magari yenu.”

Viongozi wengine waliowahimiza wakulima kufuata mwito huo wa Wainaina ni Seneta maalum Bw Isaac Mwaura na mbunge wa Gatundu Kaskazini anayefuatana na kesi mahakamani kuhusu uhalali wa kiti chake Bi Wanjiku Kibe.

Walisema kwa kauli moja wanangoja mswada huo wa kilimo cha majanichai uwasilishwe bungeni ili waupitishe mara moja.