Wakulima wa Mataara wapinga uchaguzi wa ghafla

Wakulima wa Mataara wapinga uchaguzi wa ghafla

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wa majanichai kutoka eneo la Mataara, Gatundu Kaskazini, wamepinga uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumamosi, wakidai ni haramu.

Kwanza wamesema wakati huu wa janga la Covid-19 hawafai kufanya mikusanyiko ya pamoja na kwa hivyo hawaoni haraka ya kufanya uchaguzi huo.

Mkulima Bw Peter Gicheha anadai ya kwamba wapo watu wanaotaka kuendesha uchaguzi haraka ili waingie uongozini.

Uchaguzi huo unaweza kusababisha vurugu huku watu wakiwa katika hali ya kujizuia corona.

Mkulima mwingine Bi Ruth Muthoni alisema wanataka wapewe muda ili wafikirie ni viongozi gani wangestahili kuchagua.

Alidai mtu yeyote anayetaka kuchaguliwa ni sharti aje mashinani kutafuta kura kutoka kwa wakulima.

Wakulima hao walidai ya kwamba hawakupewa ilani ya mapema kuhusu uchaguzi huo ila waliona notisi ya haraka ikieleza kuhusu uchaguzi huo.

Walitaka serikali isitishe uchaguzi huo mara moja hadi wakati Wizara ya Afya itatoa ruhusa kwa wananchi kujumuika pamoja.

Naye Bw Jesse Mungai alisema mtu yeyote anayetaka kupewa uongozi ni sharti afike mashinani na azungumze na wakulima ana kwa ana.

“Sisi kama wakulima tungetaka mambo yaendeshwe kwa utaratibu unaostahili bila kuleta vurugu,” alisema Bw Mungai.

Wakulima hao walisema uchaguzi huo ukikubaliwa kuendelea utakiuka sheria za kudhibiti corona kwa sababu watu watahatarisha maisha yao iwapo utaendelea.

Wakulima hao wenye hasira walitaka serikali kuingilia kati kuona ya kwamba hakuna uchaguzi utaendelea katika kiwanda cha chai cha Mataara.

Walisema watu wanataka kuharakisha uchaguzi ili wapate vyeo vya uongozi.

You can share this post!

Wakazi wa Gatundu Kaskazini wataka walipwe fidia

Mabinti wabwaga wavulana