Habari Mseto

Wakulima wa maziwa kulipwa Sh33 kwa lita

January 15th, 2020 1 min read

Na LEOPOLD OBI

SERIKALI imetangaza bei mpya za maziwa kwa wafugaji wadogo.

Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya Jumatano aliagiza kampuni ya New KCC inunue maziwa ya wafugaji kwa Sh33 badala ya Sh25 kwa kila lita.

Alisema hatua hiyo inalenga kuwapa motisha wafugaji ambao hulalamika kuhusu bei duni ya maziwa.

Wakati huo huo, katika kikao chake cha kwanza kama waziri wa kilimo, Bw Munya alionya wafanyabiashara dhidi ya kuagiza maziwa ya bei ya chini kutoka mataifa ya kigeni wakati wafugaji wana bidhaa hiyo kwa wingi.

“Ni makosa sana kununua maziwa kutoka nchi za nje ilhali wafugaji wana maziwa ya kutosha. Tunaomba wafanyabiashara wanunue maziwa hapa nchini,” akasema Bw Munya.

Wizara hiyo pia iliomba wakulima wasiwe na wasiwasi kuhusu nzige waliovamia nchi Desemba 28.

Bw Munya alisema serikali imeongeza maafisa wa kuangamiza wadudu hao waharibifu kando na kuimarisha ukaguzi wa maeneo yaliyo hatarini kuvamiwa pamoja na unyunyizaji dawa kutoka kwa ndege katika kaunti zilizoathirika.

Kwa mujibu wa waziri, ndege nane zaidi zitaanza kutumiwa leo kwa unyunyizaji wa dawa.

Ndege hizo zitapelekwa katika maeneo yaliyoathirika zaidi ambayo ni Garissa, Mandera na Marsabit ili kuzuia nzige kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine.

Aliongeza kuwa sekta ya kibinafsi pia imejiunga katika juhudi hizo za kuangamiza nzige katika maeneo ya mipaka ya Laikipia na Isiolo.

Alisema kwa sasa wizara haina uwezo wa kutambua kiwango cha uharibifu uliofanywa na wadudu hao wenye uwezo wa kusafiri hadi kilomita 200 kwa siku.