Habari Mseto

Wakulima wa miche Nyeri waisihi serikali ya kaunti kuwa promota wao katika mpango wa kufadhili wakulima miche ya avocado bila malipo

June 7th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KWA muda sasa baadhi ya kaunti zimekuwa zikiwapa wakulima wakazi wake miche ya miparachichi bila malipo.

Kaunti ya Nyeri na ile ya Murang’a ndizo zinaongoza katika shughuli hiyo.

Hatua hii hasa imeonekana kuchochewa na makubaliano Kenya kuuza matunda haya nchini China.

Mkataba huo ulitiwa saini Aprili 2019 na Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa China, Xi Jinping.

Ili kufanikisha mpango huo Nyeri, serikali ya kaunti hiyo inapania kufungua kiwanda kitakachokusanya maparachichi kutoka kwa wakulima.

Gavana Mutahi Kahiga alisema yatakuwa yakisafishwa, kuchaguliwa ili kuuzwa nje ya nchi. Alisema kiwanda hicho kitasaidia kuinua wakulima wa maparachichi Nyeri kimapato.

“Kupitia kugatuliwa kwa sekta ya kilimo, ni wajibu wetu kama serikali ya kaunti kuinua maisha ya wakulima,” akasema gavana Kahiga.

Mpango huo umepokelewa vyema na wakulima, wakitumai hautachochewa kisiasa ili kukwepa kero ya mawakala.

Bw Richard Maina ni mkulima wa maparachichi, miche yake pamoja na ya matunda mengine kama vile matufaha, mapera na matundadamu.

Pia, hukuza miche ya miti ya mbao, kurembesha mazingira na hata maua.

“Mpango wa serikali kuuza maparachichi ya Kenya nchini China ukifuatwa ifaavyo utatufaa pakubwa sisi wakulima,” anasema Bw Maina.

Serikali imehimizwa kuunda mashirika yatakayokuwa yakikusanya mazao ya matunda haya kutoka kwa wakulima; na Maina anapongeza jitihada za serikali ya kaunti ya Nyeri kuunda kiwanda.

Pia, amepokea vyema hatua ya serikali ya kaunti hiyo kufadhili wakulima kwa miche ya avocado bila malipo, akiihimiza kuwa mteja wake mkuu wa mimea hiyo michanga anayopanda.

Kauli yake inawiana na ya Teresah Njambi, mkuzaji wa miche ya matunda Karatina.

“Nyeri ina vijana kadhaa waliojiajiri kwa kupanda miche ya matunda. Ninapongeza hatua ya serikali kuwapa wakulima miche na ninaiomba iwe promota wetu mkuu,” anasema Bi Njambi.

Taasisi za kilimo

Mbali na wakulima, kuna taasisi za serikali za kilimo zinazotoa mbegu za miti kama vile Kefri.

Hata hivyo, Richard Maina anasema wakati mwingine taasisi hizo hukosa mbegu na hulazimika kusafiri kwa wakulima walioko nje ya Nyeri kuzitafuta.

“Zinapokosa, huzipata nje kwa bei ghali,” alalamika mkulima huyu.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, wataalamu wa kilimo wanahimiza wanazaraa kuwa na njia mbadala kupata mbegu kama vile kuenda katika viunga vya wakulima wa matunda. “Watumie mbegu za miti yenye afya na inayozalisha vyema. Miche yake lazima iwiane na hulka za miti ilikotolewa,” aelezea Daniel Mwenda, mtaalamu wa miti na masuala ya matunda.